F Meru Forest Adventure race 2025 yafana hifadhi ya shamba la miti Meru | Muungwana BLOG

Meru Forest Adventure race 2025 yafana hifadhi ya shamba la miti Meru


Na John Walter -Arusha

Mashindano ya Meru Forest Adventure Race 2025 yaliyofanyika Agosti 31, 2025, katika Hifadhi ya Shamba la Miti Meru/USA, yamevutia mamia ya washiriki kutoka ndani na nje ya mkoa wa Arusha.

Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi, ambaye pia alishiriki mbio za kilomita 10 msituni.

Akizungumza baada ya kumaliza mbio, Mwinyi amesema mashindano hayo yamechangamsha washiriki kimwili, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuongeza thamani ya utalii wa misitu.

“Ni mbio za kipekee ambazo zimenikutanisha na watu wengi,  changamoto za msitu, maporomoko ya maji na mandhari ya asili yameongeza furaha na msisimko kwa washiriki.

Niwapongeze TFS na waandaaji kwa kuendeleza falsafa ya utalii wa michezo inayosisitizwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Mwinyi.

Kwa upande wake, Xavery Thobias Chuwa wa Quality Sports Promoters alibainisha kuwa mwaka huu wameanzisha Obstacle Race yenye changamoto za viwango vya kimataifa, ikiwapa washiriki uzoefu wa kipekee na kuwavutia wageni kutalii ndani ya msitu huo.

Tukio la mwaka huu lilijumuisha michezo ya aina mbalimbali ikiwemo mbio za kilomita 5, 10 na 20, Enduro kwa pikipiki kwa wanafunzi, wa kati na wataalamu, pamoja na mashindano ya baiskeli na motocross yaliyoongeza hamasa kwa washiriki na watazamaji. Washindi walizawadiwa zawadi maalum.

Burudani za kitamaduni hazikukosekana, ambapo ngoma za Kimaasai, nyama choma na vinywaji mbalimbali vilipamba tukio, na kugeuza mashindano hayo kuwa sherehe kubwa ya kijamii na utalii.

Afisa Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Yusuf Tango, alisema lengo kuu la mashindano hayo ni kukuza utalii wa ikolojia na michezo, huku Mhifadhi Mkuu, PCO Ali D. Maggid, akibainisha mpango wa kuyapanua mashindano hayo hadi ngazi ya kimataifa ili kuongeza idadi ya washiriki na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha michezo na utalii wa asili.

Huu ukiwa ni msimu wa tatu wa Meru Forest Adventure Race, mashindano hayo yanaendelea kujidhihirisha kama jukwaa muhimu la kukuza utalii wa michezo na kuhamasisha utunzaji wa mazingira ya hifadhi za misitu nchini.

Post a Comment

0 Comments