Na John Walter-Babati
Moto mkubwa uliosababishwa na mafuta ya kukaangia chips umezuka usiku wa kuamkia leo Alhamisi, Septemba 11, 2025, katika mgahawa wa Sam Food uliopo mtaa wa Maisaka Kati, mjini Babati, mkoani Manyara, na kusababisha hasara kubwa ya mali.
Mashuhuda wamesema moto huo ulianza majira ya saa moja usiku baada ya mafuta yaliyokuwa yakitumika kukaangia chips kulipuka na kusababisha mlipuko ulioenea haraka. Samani za mgahawa huo ikiwemo meza, viti na masanduku ya soda viliteketea kwa moto.
Miongoni mwa wafanyakazi wa mgahawa huo, Samweli, ameeleza kuwa chanzo cha moto hakikuwa mtungi wa gesi kama ilivyodhaniwa awali, bali mafuta ya chips yaliyolipuka na baadaye kusababisha moto kufika kwenye mitungi ya gesi iliyokuwa ikitumika kwa mapishi na kusababisha mlipuko mkubwa.
“Hakuna madhara kwa binadamu yaliyoripotiwa kwa sasa, hakuna majeruhi wala vifo,” amesema Samweli.
Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Manyara, Joackim John Katandasa, amesema walipokea taarifa za tukio hilo majira ya saa 1:40 usiku na walifika eneo la tukio dakika tano baadaye.
“Tulifanikiwa kuuzima moto huo na kuokoa jengo la mgahawa pamoja na majengo ya jirani ambayo yalikuwa hatarini kushika moto kutokana na ukubwa wa mlipuko,” amesema Katandasa.
Mamlaka husika zimeendelea na tathmini ya uharibifu uliojitokeza huku wakazi wa Babati wakihimizwa kuchukua tahadhari zaidi wanapotumia mafuta na mitungi ya gesi majumbani na katika biashara zao ili kuepuka majanga ya aina hiyo. 


