RC Manyara azionya taasisi zinazowanyanyasa wafanyakazi


Na John Walter-Babati
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ameendelea na utaratibu wake wa kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi kupitia mfumo wa baraza maalum, unaowakutanisha walalamikaji, walalamikiwa pamoja na taasisi husika ili kupata majibu ya moja kwa moja.

Katika kikao hicho kilichofanyika Jumatano na Alhamisi kwenye ukumbi wa mikutano mkoani humo, Sendiga aliwaonya viongozi wa sekta binafsi wanaowanyanyasa wafanyakazi kwa kuwakosesha mikataba ya kazi na haki zao za msingi, akisema vitendo hivyo havitavumiliwa.

“Kuna baadhi ya viongozi wa sekta binafsi wanajiona miungu watu, wakiwatesa na kuwadhalilisha wafanyakazi. Hii tabia ni lazima iishe. Sheria zipo na zitasimamiwa,” alisisitiza RC Sendiga.

Miongoni mwa kero zilizowasilishwa katika kikao hicho ni za walimu waliowahi kufundisha katika Shule ya Aldersgate, waliodai hawajalipwa mafao yao licha ya kuitumikia shule hiyo kwa muda mrefu. Walimu hao, akiwemo aliyekuwa mkuu wa shule kwa zaidi ya miaka 15, walisema waliondolewa bila utaratibu na kuomba msaada wa serikali ili wapate haki zao.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa shule hiyo walikanusha madai hayo wakibainisha kuwa walimu hao walikuwa wakifanya kazi kwa kujitolea na si kwa mkataba rasmi.

Kufuatia mvutano huo, RC Sendiga alimuelekeza Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara kufuatilia nyaraka za shule hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe iwapo kutabainika kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za kazi.

Baraza hilo limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi mkoani Manyara, likilenga kuimarisha uwajibikaji wa taasisi za umma na binafsi.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi