Sillo abainisha Vipaumbele kwa Wananchi Babati vijijini



Na John Walter-Babati

Mgombea ubunge wa Jimbo la Babati Vijijini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Sillo, amewataja vipaumbele vyake kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya mwelekeo wa maendeleo kwa miaka mitano ijayo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, Sillo amesema vipaumbele vyake ni pamoja na ujenzi wa madaraja na barabara za viwango, upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote vya jimbo hilo.

“Barabara ni uchumi, na kwa kuwa wananchi wa Babati wengi ni wakulima na wafugaji, lazima tuhakikishe zinakuwa bora ili mazao na mifugo yao yafikishwe sokoni kwa urahisi,” alisema Sillo.

Aidha, Sillo amebainisha kuwa yote aliyoyataja yako ndani ya Ilani ya CCM ya mwaka 2025-2030, na akaongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jimbo la Babati Vijijini limepokea zaidi ya shilingi bilioni 244.97 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

“Yajayo yanafurahisha zaidi, kilichobaki sasa ni wananchi kupiga kura za kutosha, nawaomba mnipatie kura nyingi, kwa pamoja na madiwani wetu na rais wetu, ili tushirikiane kutekeleza haya yote kwa vitendo,” alisisitiza Sillo.

Uzinduzi wa kampeni hizo umefanyika kata ya Mamire na kufanywa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Joachim Muungano, huku viongozi mbalimbali wa chama wakihudhuria na kuonyesha mshikamano mkubwa.

CCM imeendelea kusisitiza kaulimbiu yake kwa uchaguzi huu kuwa Oktoba 29 ni mwendo wa kutiki, kutiki, kutiki. ✅

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi