Na John Walter-Babati
Mgombea Udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Madunga, John Noya, ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, amesema moja ya jambo la kwanza atakaloanza nalo mara baada ya kuapishwa ni kufuatilia upatikanaji wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Madunga.
Amesema hatua hiyo imelenga kuwaondolea wananchi usumbufu na gharama kubwa wanazozipata wanapolazimika kusafirisha marehemu umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Mbali na hilo, Noya ametaja vipaumbele vingine atakavyoshughulikia kwa haraka kuwa ni pamoja na kusogeza huduma ya umeme katika vitongoji, maji safi na salama pamoja na kuboresha barabara.
Amesema yote aliyoyataja yapo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030, hivyo wananchi wa Madunga wawe na imani kuwa yatafanyiwa kazi kwa vitendo.
Aidha, amewataka wananchi wa Kata ya Madunga kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29 na kumpa kura ya ndiyo, akisisitiza kuwa kata hiyo haina mgombea mwingine zaidi ya CCM.
Katika uzinduzi wa kampeni hizo, mgeni rasmi ambaye pia ni Mgombea Udiwani wa Kata ya Bashnet, Jovitha Mandoo, alisema ifikapo Oktoba 29 Tarafa ya Bashnet itatoa kura nyingi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wa CCM.
Mandoo alisema John Noya ni kiongozi makini, mpenda maendeleo na mfuatiliaji wa karibu wa changamoto za wananchi, hivyo anastahili kupewa ridhaa ya kuendelea kuwatumikia wananchi wa Madunga.