F Sumaye awaunganisha Wana CCM Mbulu Vijijini, avunja makundi ya kisiasa | Muungwana BLOG

Sumaye awaunganisha Wana CCM Mbulu Vijijini, avunja makundi ya kisiasa


Na John Walter-Mbulu

Waziri Mkuu mstaafu, Mheshimiwa Frederick Sumaye, leo ameweka sawa wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbulu Vijijini kwa kuwataka kuvunja makundi yaliyokuwa yamejitokeza ndani ya chama na kuondoa chuki, badala yake kushirikiana kwa dhati kusaka kura za ushindi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu.

Akizungumza kwenye kikao cha ndani cha CCM kilichofanyika Dongobesh, Sumaye amesema ni jambo baya kwa wanachama kumnyanyapaa mgombea aliyepitishwa na chama, akisisitiza kuwa vitendo hivyo havileti taswira njema kwa CCM mbele ya jamii. 

“Kwa makubwa yaliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka minne, ikiwemo maridhiano na vyama vya upinzani, hakuna sababu ya kugawanyika. Tunapaswa kuwa kitu kimoja,” alisema.

Katika kikao hicho, Sumaye alifanikiwa kuwakutanisha mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Mbulu Vijijini, Dkt. Emmanuel Nuas, pamoja na mbunge mstaafu Flatei Gregory Massay, ambapo walipeana mikono na kuahidi kushirikiana kikamilifu kusaka kura za chama hicho. 

Hatua hiyo imevunja makundi yaliyokuwepo, jambo lililopongezwa na wajumbe wa kamati ya siasa wilaya.

Wajumbe hao, wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na mgombea udiwani Kata ya Dinamu, Joseph Mandoo, walimpongeza Flatei kwa moyo wake wa busara na uaminifu kwa CCM licha ya changamoto za kisiasa alizopitia.

Flatei, ambaye aliwahi kuongoza Jimbo la Mbulu Vijijini kwa mafanikio kwa zaidi ya miaka 10 na baadaye kujiunga na ACT-Wazalendo baada ya jina lake kikatwa na kamati kuu, amerudi CCM wiki chache zilizopita baada ya mazungumzo ya ndani ya chama yakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Steven Wasira

Akizungumza leo, Flatei amesema: “sina kinyongo tena, na niko tayari kushirikiana bega kwa bega na Dkt. Nuas kuhakikisha ushindi wa chama.”

Kwa upande wake, Dkt. Nuas alimhakikishia Flatei kuwa watashirikiana katika kila hatua ya kampeni na kuleta ushindi wa kishindo kwa CCM.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Namelok Sokoine, naye amewataka wanachama wote kuungana na kusahau makundi ya zamani kwa ajili ya mshikamano wa chama.

Aidha, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima, amesisitiza kuwa uchaguzi wa ndani ya chama umekwisha, na sasa ni wakati wa kuunganisha nguvu zote kusaka kura za ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.

Jimbo la Mbulu Vijijini na Mjini kuna jumla ya kata 35, ambapo kwa mujibu wa Katibu wa CCM Wilaya hiyo, wagombea wa udiwani katika kata 23 tayari wamepita bila kupingwa.

Post a Comment

0 Comments