F Dkt. Samia aahidi Barabara za Lami na Kudhibiti Wanyama Wakali Manyara. | Muungwana BLOG

Dkt. Samia aahidi Barabara za Lami na Kudhibiti Wanyama Wakali Manyara.


Na John Walter, Babati

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kujenga barabara kuu na za vijijini kwa kiwango cha lami mkoani Manyara endapo ataendelea kupewa ridhaa ya kuongoza Taifa.

Akihutubia wananchi wa Manyara Oktoba 4, Dkt. Samia amesema serikali yake itaendelea kufungua mikoa kwa mtandao wa barabara za lami ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kukuza uchumi.

Barabara alizotaja kujengwa kwa kiwango cha lami ni Simanjiro–Kongwa, Garbab–Mbulu, Mogitu–Haydom na Nangwa/Gisamgalang–Kongwa. 

Aidha, amesisitiza serikali itaimarisha pia barabara za vijijini ili wakulima wasipate shida kusafirisha mazao yao sokoni.

Katika sekta ya utalii, Dkt. Samia ameahidi kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni 5.3 waliorekodiwa miaka mitano iliyopita hadi kufikia zaidi ya milioni nane. Alisema hatua hiyo itachochea ukuaji wa pato la taifa na kuinua kipato cha wananchi.

Aidha, amegusia changamoto ya wanyama wakali wanaosumbua vijiji vilivyopo jirani na hifadhi za taifa, akiahidi serikali itajenga vituo vya kudhibiti wanyama hao na kushirikisha vijana wa vijijini pamoja na maafisa wa TAWA na TAWIRI ili kulinda maisha na mali za wananchi.

“Hatua tutakazochukua ni kujenga vituo vya kudhibiti wanyama wakali na tutachukua vijana wa vijijini wasaidiane na maafisa wa TAWA na TAWIRI,” alisema Dkt. Samia.

Awali, wagombea ubunge wa majimbo ya mkoa wa Manyara walimweleza kero na maombi yao, akiwemo Edward Ole Lekaita (Kiteto), James Ole Millya (Simanjiro), Dkt. Emmanuel Nuwas (Mbulu Vijijini), Zacharia Isaay (Mbulu Mjini) na Emmanuel Khambay (Babati Mjini) waliotaka barabara kuu ziwekwe kwa kiwango cha lami.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Babati Vijijini, Daniel Sillo, aliomba vijiji 10 vilivyopo jirani na hifadhi za taifa visaidie kuondolewa tatizo la wanyama wakali, jambo ambalo Dkt. Samia aliahidi kulitafutia suluhu ya kudumu.

Post a Comment

0 Comments