F Dkt Samia atoa neno la faraja kwa wakulima wa mbaazi | Muungwana BLOG

Dkt Samia atoa neno la faraja kwa wakulima wa mbaazi



Na John Walter-Hanang
Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan amewatoa hofu wakulima wa zao la mbaazi mkoani Manyara, baada ya kulalamikia kushuka kwa bei ya zao hilo kati ya shilingi 700 hadi 800 kwa kilo.

Akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo kwenye Kata ya Katesh, Wilaya ya Hanang’, Dkt. Samia amesema serikali inalifuatilia suala hilo kwa karibu na tayari mazungumzo yanaendelea na nchi ya India ili kufanikisha upatikanaji wa soko la mbaazi.

“Zao la mbaazi limelimwa maeneo mengi duniani, na bei yake ya sasa ni takribani asilimia 70 ya bei ya mwaka uliopita. Hata hivyo, msivunjike moyo, serikali ipo pamoja nanyi kuhakikisha mnapata masoko yenye tija,” alisema Dkt. Samia.

Ameongeza kuwa sekta ya kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, hivyo serikali ya CCM itaendelea kuweka mazingira bora ya masoko ya mazao, kuongeza thamani kupitia viwanda vya ndani na kuwahakikishia wakulima kuwa jasho lao halitapotea.

Kwa upande wao, baadhi ya wakulima waliohudhuria mkutano huo wamesema ujumbe wa faraja kutoka kwa Dkt. Samia umewatia moyo na wana imani kuwa jitihada za serikali zitaboresha soko la mbaazi na kuwaletea maendeleo endelevu.

Post a Comment

0 Comments