F Nyumba Salama Butiama waomba kukabiliana na changamoto ya dharura | Muungwana BLOG

Nyumba Salama Butiama waomba kukabiliana na changamoto ya dharura


KITUO  cha Nyumba Salama wilayani Butiama kimetoa ombi kwa wafadhili kusaidia upatikanaji wa gari la dharura ili kukabiliana na changamoto ya usafiri, hasa nyakati za usiku, kwa ajili ya kuwaokoa wasichana wanaokimbia ukeketaji na ukatili wa kijinsia.

Ombi hilo lilitolewa na msomaji wa risala, Veronica Lucas, mbele ya mgeni rasmi, Balozi wa Poland nchini Tanzania,Sergiusz Woiski, wakati wa uzinduzi wa baadhi ya majengo mapya ya Nyumba Salama uliofanyika jana.

"Sisi wasichana tunaokaa kambini Nyumba Salama baada ya kukimbia ukeketaji na ukatili wa kijinsia, tunakumbwa na changamoto kubwa ya usafiri. Tunapougua usiku, hakuna gari la kutupeleka hospitalini. Matron analazimika kumbeba mgonjwa mgongoni hadi hospitali ili kuokoa maisha. Wakati mwingine tunapokuwa uraiani kipindi cha ukeketaji, tunashindwa kupata msaada wa haraka kutokana na ukosefu wa gari. Mimi mwenyewe nilinusurika kukeketwa lakini wenzangu wawili walikeketwa. Kama gari lingekuwepo, wote tungeokoka," alisema Veronica kwa uchungu.

Naye mkazi wa Butiama, Esther Moroli, alisema ukatili wa kijinsia ni tatizo kubwa linaloathiri maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nyumba Salama, Rhobi Samweli, alishukuru Ubalozi wa Poland na wadau wengine kwa kufanikisha ujenzi wa kituo hicho salama kwa wasichana wanaokimbilia kukwepa ukatili.

Domina Walter, Mkurugenzi Msaidizi wa Nyumba Salama, alisema kuwa pamoja na mazingira kuwa salama, changamoto kubwa ni ukosefu wa gari la dharura kwa ajili ya kuwahudumia watoto wagonjwa, kuwarudisha makwao wanapomaliza kambi, au kuingilia kati kesi za ukatili.

Domina alieleza kuwa tangu mwaka 2017 hadi 2025, Nyumba Salama imesaidia jumla ya wasichana 3,277 waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni. Kati yao, wasichana 1,232 walifanikiwa kurejea shuleni kuendelea na masomo, huku wasichana 3,262 wakipatiwa mafunzo ya ujuzi wa maisha. Pia, zaidi ya wananchi 100,000 wameelimishwa kuhusu madhara ya ukatili na mbinu za kupambana nao.


Post a Comment

0 Comments