F RC Manyara atoa onyo dhidi ya wanaopanga vurugu kipindi cha Uchaguzi | Muungwana BLOG

RC Manyara atoa onyo dhidi ya wanaopanga vurugu kipindi cha Uchaguzi

Na John Walter-Babati

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amewaonya wananchi na makundi yote katika jamii kuepuka vitendo vyovyote vya vurugu, uchochezi au uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Oktoba 21, 2025, Sendiga amesema maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri huku hali ya usalama ikiwa imetulia katika mkoa mzima wa Manyara.

Amesema hadi sasa hakuna taarifa yoyote kuhusu mtu au kikundi kinachopanga kufanya vurugu, na kusisitiza kuwa utulivu na amani ni jukumu la kila mmoja.

“Tunawataka wananchi wote wawe watulivu, waende wakapige kura kwa amani na baada ya kupiga kura warudi majumbani mwao kusubiri matokeo. Amani na utulivu ni vitu vya lazima, haviepukiki,” amesema Sendiga.

Ameongeza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimeimarisha ulinzi kabla, wakati na baada ya uchaguzi, ili kuhakikisha wananchi wote wanashiriki zoezi hilo la kikatiba bila hofu.

Sendiga pia ametoa wito kwa makundi yote ya kijamii, wakiwemo viongozi wa dini, vijana, wanawake na wazee, kuhamasishana kwenda kupiga kura kwa wingi na kulinda amani ya nchi.

Aidha, ametoa onyo kali kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, hususan kwenye makundi ya WhatsApp, kuepuka kusambaza taarifa za uchochezi, maneno ya kuwatisha wananchi au kuvuruga utaratibu wa uchaguzi.

“Tujilinde dhidi ya kauli za uchochezi. Mitandao itumike kwa mambo ya kujenga, si kuvuruga,” amesema.

Mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa siku ya Jumatano, Oktoba 29, ambayo ni siku ya uchaguzi, itakuwa siku ya mapumziko ya kitaifa, hivyo wananchi wanapaswa kutumia muda huo kushiriki kupiga kura na kudumisha utulivu hadi matokeo yatakapotangazwa rasmi.

Post a Comment

0 Comments