Kamati ya utekelezaji ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Njombe imeendelea na ziara zake za kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ambapo Octoba 5 timu ya ushindi ya UWT imefanya mikutano ya kampeni katika kata za Manda, Luhuhu, Masasi na Mkomang’ombe.
Katika mikutano hiyo, Mgombea Mteule wa Ubunge wa Viti Maalumu, Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana, aliambatana na wajumbe wa Timu ya Ushindi ya UWT Mkoa wa Njombe akiwemo Irene Sanga, Salma Kikoti na Joyce Gakye.
Wajumbe hao wamesisitiza umuhimu wa amani kama nguzo kuu ya maendeleo ya taifa, wakibainisha kuwa wanawake wana nafasi kubwa ya kulinda na kudumisha amani hiyo. Walihimiza wanawake kote nchini kuwachagua viongozi bora kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakisema ndiko viongozi imara na wenye dira ya maendeleo hupikwa.
Akizungumza na wanawake wa kata hizo, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Timu ya Ushindi wa UWT Mkoa wa Njombe, Dkt. Barozi Pindi Chana, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Timu ya Ushindi, Dkt. Scholastika Kevela, alisema miradi mikubwa ya maendeleo iliyoanzishwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itaendelezwa na kukamilishwa endapo wananchi wataendelea kukipa chama hicho ridhaa ya kuongoza katika ngazi zote — kuanzia udiwani, ubunge hadi urais.
“Wananchi wanapaswa kuwa na uchungu na maendeleo ya nchi yao kwa kuwachagua viongozi wazalendo na waadilifu watakaoipeleka Tanzania mbele,” alisema Dkt. Barozi kwa niaba ya Dkt. Kevela.
Aidha, Dkt. Barozi ameomba kura za ndiyo kwa Mgombea wa Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge Josephat Kamonga, pamoja na wagombea wa udiwani wa kata hizo tatu: Yohana Godfrey, Chale William Kunyanja, na Daniel Mahundi. Alisema wagombea hao wanauelewa mzuri wa changamoto za wananchi na wamejipanga kuzipatia ufumbuzi wa kudumu.
Kwa upande wao, wanawake wa UWT kutoka kata hizo tatu walitoa pongezi kwa siasa safi na za kistaarabu zinazoendeshwa na Chama Cha Mapinduzi. Waliwahimiza wanachama na wananchi kwa ujumla kuendelea kufanya siasa zenye heshima, umoja na upendo.
0 Comments