Wakulima na wasindikaji wadogo wa zao la zabibu mkoani Dodoma wamepatiwa mafunzo maalum ya kukuza ujuzi katika mlolongo wa thamani wa zao hilo, yakiwemo masuala ya uvunaji, uhifadhi, uongezaji thamani na mbinu za kutafuta masoko ya zabibu na bidhaa zake.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Oktoba 20, 2025 Hombolo, jijini Dodoma, Afisa Kazi Mkuu Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Neema Moshi, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ujuzi na maarifa kwa wakulima na wafanyakazi ili kuendana na mabadiliko ya kisayansi, kiteknolojia na kiuzalishaji.
Mafunzo haya yanawezesha nguvu kazi ya taifa kupata ujuzi na maarifa yanayokidhi mahitaji ya soko la Ajira, kuboresha tija na kuongeza ubora wa bidhaa pamoja na huduma wanazozalisha, amesema.
Awali, akizungumza Mkulima wa Zabibu kutoka Hombolo, Bi. Rachel Mushi, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kujifunza mbinu bora za uhifadhi na usindikaji wa zabibu jambo litakalomwezesha kuongeza kipato kupitia uzalishaji wa bidhaa zenye ubora wa juu.
Awali tulikuwa tunauza zabibu ghafi pekee, lakini sasa tumejifunza kuzalisha juisi, jamu na mvinyo wa kienyeji. Hii itatufungulia fursa nyingi zaidi za kipato. Tunashukuru sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutuletea mafunzo haya muhimu, amesema Bi. Mushi.
Naye Bw. Daniel Mgonja, msindikaji mdogo wa zabibu kutoka kijiji cha Nzuguni, amesema kupitia mafunzo hayo amepata uelewa kuhusu ubora wa vifungashio na namna ya kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, inayolenga kuwajengea uwezo wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali, ikianzia na wakulima na wasindikaji wadogo wa zao la Zabibu. Aidha, yanatolewa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), ambapo jumla ya Wakulima 70 wamepatiwa ujuzi.
0 Comments