Na John Walter-Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amesema utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote umeanza rasmi mkoani humo kwa kutoa bima za afya kwa wazee pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mfuko huo, kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.
Mhe. Sendiga ameyasema hayo Januari 27, 2026, mjini Babati, wakati wa kikao chake na Waganga Wakuu wa Halmashauri zote saba za Mkoa wa Manyara, Makatibu wa Afya, Wakuu wa Idara za Mkoa pamoja na watumishi wa afya kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza katika kikao hicho, amesema tayari Mkoa umeanza utekelezaji wa awamu ya kwanza kwa makundi muhimu yaliyoainishwa, yakiwemo wazee, watoto, wajawazito pamoja na kaya zisizojiweza.
“Mpaka sasa tunavyozungumza, tayari tumeshatoa bima za afya kwa wazee, wameshapata kadi zao na wapo tayari kuanza kupata huduma za matibabu, tumeshafanya utambuzi na tumeshatoa kadi saba kati ya kadi tisa zinazotakiwa kutolewa katika kituo cha wazee cha Magugu, ambako wazee hao hawana watu wa kuwasaidia,” alisema Mhe. Sendiga.
Aidha, ameeleza kuwa kila kaya yenye watu sita—baba, mama na watoto wanne—inaweza kupata Bima ya Afya kwa gharama ya ruzuku ya shilingi 150,000 kwa mwaka mzima.
Ameongeza kuwa mpango wa Mkoa ni kufikia kaya laki nne na elfu tatu (403,000) ili ziingie kwenye mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote na pia zipatiwe elimu kuhusu faida za mpango huo.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa ametoa maelekezo kwa watendaji husika kuhakikisha elimu ya Bima ya Afya inawafikia wananchi wote kupitia njia mbalimbali ikiwemo mikutano ya hadhara, redio, vikao vya kijamii, mashuleni na hata mtu kwa mtu, ili kila kaya katika kila Halmashauri iweze kufikiwa.
Pia amezitaka Halmashauri zote kusimamia kwa karibu uboreshaji wa huduma za afya na kuongeza ubunifu ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana katika vituo vya afya, zahanati na hospitali za Mkoa.
Amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kupata kero yoyote katika upatikanaji wa huduma, huku akihimiza kuhakikisha dawa zinapatikana muda wote bila visingizio.
Kwa ujumla, utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote mkoani Manyara unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote, hususan makundi maalum, na kupunguza gharama za matibabu kwa jamii.
.heic)
.heic)
.heic)
.heic)
.heic)
.heic)
0 Maoni