F Fountain Gate FC Yahama Manyara, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Babati Wabaki Bila Timu ya Ligi Kuu | Muungwana BLOG

Fountain Gate FC Yahama Manyara, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Babati Wabaki Bila Timu ya Ligi Kuu


Na John Walter-Manyara

Klabu ya Fountain Gate Football Club (FGFC) imetangaza rasmi kuhamisha makao makuu na kituo chake cha uendeshaji wa shughuli za klabu kutoka Mkoa wa Manyara kwenda Mkoa wa Arusha, hatua inayofungua ukurasa mpya katika historia ya klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kupitia taarifa yake rasmi, uongozi wa Fountain Gate FC umetoa shukrani za dhati kwa wakazi wa Mkoa wa Manyara, hususan wananchi wa mjini Babati, mashabiki waaminifu, wadau na viongozi wa serikali kwa ushirikiano mkubwa na mchango mkubwa walioutoa tangu klabu hiyo ilipoanza kutumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kama uwanja wake wa nyumbani.

Uongozi wa klabu umeeleza kuwa kipindi chote walichokuwepo Manyara kimekuwa cha mafanikio, yakichangiwa kwa kiasi kikubwa na sapoti ya jamii ya Babati ambayo ilijitokeza kwa wingi, ikiwemo kusafiri na timu kwenda mikoa mbalimbali ilipokuwa ikicheza mechi zake za Ligi Kuu.

Sababu za kuhamia Arusha zimeelezwa kuwa ni pamoja na kufungua fursa zaidi za kibiashara na uwekezaji, pamoja na sababu za kiufundi, hususan upatikanaji wa miundombinu bora kwa ajili ya maendeleo ya timu.

Hata hivyo, uongozi wa FGFC umefafanua kuwa Mkoa wa Manyara utaendelea kuwa makao ya Taasisi ya Fountain Gate, ambapo timu za vijana na timu ya wanawake zitaendelea kutumia miundombinu ya michezo ikiwemo Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kwa ajili ya mafunzo na mashindano yao.

Aidha, klabu imetangaza kuwa tarehe 06 Februari 2026, Fountain Gate FC itapokelewa rasmi Mkoani Arusha katika hafla itakayofanyika chini ya uongozi wa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuanzia saa 5:00 asubuhi.

Hatima ya Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Babati

Baada ya kuondoka kwa Fountain Gate FC, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo mjini Babati sasa unabaki bila timu ya Ligi Kuu itakayoutumia kama uwanja wa nyumbani. Hali hiyo imeibua maswali mengi miongoni mwa wadau wa michezo na mashabiki wa soka mkoani Manyara.

Maswali yanayoibuka ni pamoja na:

  • Je, uwanja huo utatumika kwa shughuli zipi sasa?
  • Ni timu zipi zitapewa nafasi ya kuutumia?
  • Je, kuna mpango wa kuhamishia timu nyingine ya ligi kubwa mjini Babati?
  • Hatima ya mashabiki waliokuwa wakijitokeza kwa wingi kuujaza uwanja huo itakuwaje?

Kwa sasa, mamlaka za michezo mkoani Manyara bado hazijatoa kauli rasmi kuhusu mustakabali wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, lakini wachambuzi wa soka wanaona kuwa hatua hiyo ni changamoto na pia fursa ya kuendeleza soka la mkoa huo kupitia timu mpya au uwekezaji wa kimichezo.

 

Chapisha Maoni

0 Maoni