Na John Walter-Manyara
Daraja la
wapita kwa miguu la Tipri katika Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, limeendelea
kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo baada ya kumaliza changamoto ya
mawasiliano iliyodumu kwa muda mrefu.
Kabla ya
ujenzi wa daraja hilo la kamba lililosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini
na Mijini (TARURA), wananchi walikosa njia salama ya kuvuka kutoka eneo moja
kwenda jingine, hali iliyosababisha huduma muhimu kama elimu, afya na biashara
kukwama.
Wanafunzi
wa Shule ya Msingi Tipri wanasema daraja hilo limewarahisishia kufika shuleni
kwa wakati na kwa usalama zaidi.
Mwalimu
wa shule hiyo, Josephine Dangati, anabainisha kuwa daraja hilo limepunguza
utoro na kuchelewa kwa wanafunzi, jambo linalochangia kuboresha ufaulu wa
kitaaluma.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa kitongoji cha Tsawa, kijiji cha Tsawa, Isaack
Gwandu, amesema ujenzi wa daraja hilo limeongeza furaha kwa kijamii na
kuchochea shughuli za kiuchumi kwa kuwa wananchi sasa wanavuka kwa urahisi
kusafirisha bidhaa na kupata huduma mbalimbali.
Akizungumzia
mradi huo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbulu, Mhandisi Nuru Hondo, amesema
daraja hilo ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya usafiri
vijijini ili kurahisisha maisha ya wananchi likijengwa Kwa shilingi Milioni
147.
Naye
Meneja wa TARURA Mkoa wa Manyara, Mhandisi Salim Bwaya, amesisitiza kuwa TARURA
itaendelea kujenga na kuboresha madaraja na barabara ili kuhakikisha
mawasiliano yanakuwa ya uhakika mwaka mzima.
Kwa sasa,
wananchi wa Tipri wanaeleza furaha yao huku wakilitaja daraja hilo kama alama
ya maendeleo na matumaini mapya kwa jamii yao.
0 Maoni