Na John Walter-Manyara
Katibu wa
NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Rabia
Abdallah Hamid, kwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga,
wamewahimiza wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili
kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa uhakika.
Wameyasema
hayo wakati wakizungumza na mamia ya wananchi wa Kata ya Gidahababieg, Wilaya
ya Hanang, katika maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi yaliyofanyika
mkoani Manyara.
Akizungumza
katika mkutano huo, Ndugu Rabia Abdallah Hamid amesema dhamira ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha
kila Mtanzania anakuwa na uhakika wa kupata matibabu pindi anapokumbwa na
dharura za kiafya kupitia mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Ameeleza
kuwa ugonjwa haubishi hodi, hivyo kuwa na bima ya afya ni kinga muhimu kwa
wananchi kwani huwapa uhakika wa matibabu wakati wowote bila changamoto za
kifedha.
Aidha
amewahimiza wananchi kumuunga mkono Rais Dkt. Samia katika utekelezaji wa
mpango huo ili kuimarisha ustawi wa afya zao.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amesema utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika mkoa wa Manyara unaendelea kwa kishindo kwa
asilimia 100.
Ametolea
mfano utekelezaji wa ahadi za Rais Dkt. Samia katika siku 100 za awali za
uongozi wake, hususan katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya
kupitia kuanzishwa kwa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Mhe.
Sendiga amesema kuwa mpango huo tayari umeanza kutekelezwa mkoani Manyara,
ambapo wananchi wanaendelea kupewa elimu kuhusu umuhimu wa bima ya afya, huku
wanufaika wa makundi maalum tayari wakishapatiwa kadi zao za bima.
Viongozi
hao wameeleza kuwa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni mkombozi mkubwa kwa
wananchi, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakishindwa kupata
matibabu au hata kuchukua miili ya wapendwa wao hospitalini kutokana na kukosa
fedha.
Maadhimisho
hayo yalifanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Tumechagua Umoja na Amani kwa
Maendeleo ya Taifa Letu.”


0 Maoni