Na John Walter-Manyara
Halmashauri
ya Wilaya ya Babati imepata gari jipya kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa
shughuli za utawala pamoja na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya
hiyo.
Akilitambulisha
gari hilo leo katika kikao cha Timu ya Menejimenti ya Halmashauri, Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Bi. Anna Mbogo, amesema kuwa gari
hilo limetolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi wa Ofisi
ya Mkurugenzi Mtendaji.
“Serikali
Kuu imetuletea gari lenye namba ya usajili SM 44487 kwa ajili ya shughuli za
utawala. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutupatia gari hili,” amesisitiza Bi.
Mbogo.
Ameeleza
kuwa ujio wa gari hilo umefika katika kipindi muafaka ambapo Halmashauri ina
majukumu mengi ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo pamoja na shughuli
mbalimbali za kiutawala, hivyo litasaidia kuongeza ufanisi na kuwahudumia
wananchi kwa wakati.
Gari hilo
linatarajiwa kuwa chachu katika kuboresha usimamizi wa miradi ya maendeleo na
kuimarisha utendaji wa Halmashauri kwa ujumla.
