F RC Manyara Akemea Vikali Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia Mkoani Humo. | Muungwana BLOG

RC Manyara Akemea Vikali Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia Mkoani Humo.

Na John Walter-Manyara

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga, amekemea vikali vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kujitokeza mkoani humo, akisisitiza kuwa vitendo hivyo havikubaliki katika jamii inayojali utu na haki za binadamu.

Akizungumza kama mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), yaliyofanyika katika Ukumbi wa Manyara Hall, Magugu wilayani Babati, Sendiga amesema ukatili wa kijinsia bado ni changamoto kubwa na inayotia aibu kwa Mkoa wa Manyara.

Amesema kuwa kwa mwaka uliopita pekee, visa 8,490 vya ukatili wa kijinsia viliripotiwa mkoani Manyara, hali inayoonesha umuhimu wa jamii kuendelea kupinga vitendo hivyo kwa nguvu zote.

“Wakinamama tukatae ukatili kwa nguvu. Haipaswi kuwa sehemu ya maisha au ndoa zetu. Ukatili wowote ni ukiukwaji wa haki za binadamu,” alisema RC Sendiga.

Aidha, amesema baadhi ya wanawake wamekuwa wakiona ukatili kama jambo la kawaida katika maisha yao ya ndoa, jambo ambalo linapaswa kukomeshwa kupitia elimu na ujasiri wa kuripoti wahusika.

RC Sendiga pia amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi ni imara chini ya Mwenyekiti wake wa Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hali inayochangia hata jumuiya zake kuendelea kuwa imara na zenye mwelekeo wa kuhudumia jamii.

Katika tukio hilo, Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Mkoa wa Manyara, chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Fatuma Tsea, waliadhimisha sherehe za miaka 49 ya kuzaliwa CCM katika Tarafa ya Mbugwe kwa kutoa misaada mbalimbali kwa makundi yenye uhitaji, hatua iliyotajwa kuwa ni ishara ya utu na mshikamano wa kijamii.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Fatuma Tsea, amesema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto ya ukatili wa kijinsia, vitendo hivyo vinaendelea kupungua, kutokana na juhudi za Mkuu wa Mkoa kutoa elimu kwa jamii na kusimamia sheria zichukue mkondo wake dhidi ya wahusika.

Katika hafla hiyo, Bi. Lucy Maanda diwani wa viti maalum ametajwa kuwa kinara wa mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Wilaya ya Babati, kutokana na mchango wake mkubwa katika kupaza sauti na kuhamasisha jamii kupinga ukatili.

Maadhimisho hayo yalibeba kauli mbiu ya miaka 49 ya kuzaliwa CCM mwaka 2026 isemayo:
“Tumechagua Umoja na Amani kwa Maendeleo ya Chama Chetu.”

 

Chapisha Maoni

0 Maoni