Na John Walter-Manyara
Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Rabia Abdallah Hamid, ametembelea miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ na wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang’ (Tumaini), ikiwa ni sehemu ya kilele cha maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika mkoani Manyara.
Katika ziara hiyo, Ndugu Rabia alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri, mradi unaotarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 36 kwa gharama inayozidi shilingi bilioni tano.
Pembeni ya jengo hilo pia kunajengwa uwanja wa michezo mbalimbali wa halmashauri utakaotumika kukuza michezo na kuimarisha afya za wananchi.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, mgeni rasmi Ndugu Rabia Abdallah Hamid amepongeza juhudi za uongozi wa wilaya na wadau mbalimbali katika kutekeleza miradi ya maendeleo, akisisitiza umuhimu wa ubunifu na usimamizi madhubuti ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.
Maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi kwa mkoa wa Manyara yamefanyika leo wilayani Hanang’, yakihusisha ambapo katika wiki nzima zilifanyika shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo.