Jarida la Axios limemnukuu mwandishi wake, Barack Ravid, akisema kuwa Rais wa Marekani Donald Trump anasema yuko karibu kufanya uamuzi mzito kuhusu kuanzisha upya mashambulizi makubwa dhidi ya Iran.
Kulingana na Axios, Donald Trump alisema katika mazungumzo ya simu na Bw. Ravid: "Nina uamuzi mkubwa mbele yangu. Je, nichukue hatua na kuwaangamiza [serikali ya Iran] au la? Ni uamuzi mkubwa. Chaguzi zote zipo mezani."
Kauli hizi zinakuja wakati Rais wa Marekani akitarajiwa kukutana na viongozi wa Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE), Qatar, Bahrain, Kuwait, na Oman siku ya Jumanne, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa jijini New York; mkutano unaotarajiwa kujikita katika mustakabali wa mzozo na Iran.
Bw. Trump anasema ana mpango wa kutumia mkutano huo kutathmini misimamo ya mataifa ya Ghuba kabla ya kuamua hatua zake zinazofuata.
Alimwambia Barak Ravid: "Nataka kujua hali yao (nchi za Ghuba) ikoje. Siku zote tumekuwa tukiwaunga mkono na kuwalinda."
Wakati huo huo, ripoti zinaonyesha kuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, ameviagiza vikosi vya Marekani katika Mashariki ya Kati kujiandaa kikamilifu kwa uwezekano wa kurejea kwenye mapigano makali kabla ya mwisho wa mwaka.
Alipoulizwa ikiwa ana mpango wa kukutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, jijini New York wiki ijayo, Bw. Trump alisema: "Huenda."
