F Upungufu wa Madawati 432 Wabainishwa Magugu, Wananchi Wajipanga Kuchangia Maendeleo. | Muungwana BLOG

Upungufu wa Madawati 432 Wabainishwa Magugu, Wananchi Wajipanga Kuchangia Maendeleo.

 


Na John Walter-Babati

Mkutano wa hadhara wa kusoma mapato na matumizi ya Kijiji cha Magugu umebaini upungufu wa madawati 432 katika shule tano za kijiji hicho, hali inayohitaji zaidi ya shilingi milioni 34 ili kuziba pengo hilo.

Mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji, Loya Amos, uliwakutanisha wananchi na viongozi wa kijiji kujadili hali ya maendeleo pamoja na vipaumbele vinavyohitaji utekelezaji wa haraka.

Wakichangia hoja katika mkutano huo, wananchi wamesema maendeleo ni yao na wako tayari kushiriki kikamilifu endapo watawekewa utaratibu rafiki na wazi utakaowezesha kuwashawishi kuchangia miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, uongozi wa kijiji kupitia mwenyekiti na kamati ya maendeleo uliwahakikishia wananchi kuwa utazungumza kwanza na wadau wa maendeleo ili kutafuta msaada, na kiasi kitakachobaki ndipo wananchi watashirikishwa kuchangia.

Hatua hiyo ilipokelewa na kuungwa mkono na wanakijiji waliohudhuria mkutano huo.

Viongozi wa kijiji wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na uongozi katika kutatua changamoto za elimu, wakieleza kuwa upatikanaji wa madawati ya kutosha utaboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

 



Chapisha Maoni

0 Maoni