Na John Walter -Manyara
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Peter Toima, amesema chama hicho hakihalalishi uwepo wa makundi ya wanachama na viongozi ndani au nje ya chama, akieleza kuwa tabia hiyo inaleta mgawanyiko na kudhoofisha mshikamano wa chama.
Akizungumza Aprili 11, 2026 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Manyara kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Ofisi za CCM Mkoa, Toima amesema ingawa wakati wa uchaguzi makundi yanaweza kujitokeza pale wanachama wanapowania nafasi mbalimbali za uongozi, Katiba na taratibu za chama hazitambui wala kuruhusu makundi ya aina hiyo kuendelea nje ya kipindi hicho.
Amesema makundi hayo ni hatari kwa ustawi wa chama kwani hugawa wanachama, hujenga chuki na kuharibu msingi wa umoja uliopo ndani ya CCM.
“Tofauti za makundi zinaharibu chama. Viongozi wote waliopo madarakani bado wana nafasi zao za uongozi, hivyo hakuna sababu ya watu kuanza kutengeneza safu zao mapema kwa ajili ya kutafuta nafasi,” amesema Toima.
Aidha, amewataka wanachama wanaojihusisha na kupanga makundi kuacha mara moja, akisisitiza kuwa huu ni mwaka wa kazi na wa kukijenga chama kupitia ushirikiano, kusikiliza wananchi na kuwaletea maendeleo badala ya kujikita katika siasa za makundi.
Toima amesema watu wanaoendelea kuunda makundi wanachochea vurugu na kujenga uadui dhidi ya viongozi waliopo madarakani pamoja na ndani ya chama, jambo ambalo halitavumiliwa na CCM Mkoa wa Manyara.
“Chama hakiwezi kukaa kimya kutazama mambo kama hayo. Kuna watu wanakitumia chama kama daraja la kupata vyeo, lakini hawana mapenzi ya dhati kwa chama, ndiyo maana wengi wao hushindwa kufanya kazi na hawajui misingi ya CCM,” amesema.
Ameongeza kuwa chama kinaona na kufuatilia kila kinachoendelea, hivyo hakuna haja kwa wanachama kujisumbua kutafuta nafasi kwa njia zisizo halali badala ya kufanya kazi kwa bidii ndani ya chama na kwa wananchi.
Kauli hiyo imekuja wakati CCM Mkoa wa Manyara ikiendelea kusisitiza nidhamu, mshikamano na uwajibikaji kwa viongozi na wanachama wake katika utekelezaji wa majukumu ya chama na maendeleo ya wananchi.

0 Maoni