Na Rebeca Duwe, Tanga
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Tanga umesema kuwa miradi yote itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu imegharimu takribani shilingi bilioni 5, huku baadhi ya miradi ikitarajiwa kuzinduliwa na mingine kuwekewa mawe ya msingi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Tanga, George Tarimo, alisema kuwa kuna miradi minane itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu katika wilaya za Kilindi, Pangani, Handeni, Korogwe, Lushoto, Bumbuli, Muheza na Jiji la Tanga.
Tarimo alisema kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Mwenge wa Uhuru utapitia mradi wa daraja lililopo kwenye barabara ya Mapanga–Mlingotini, ambao umefikia hatua ya ujenzi wa Box Culvert.
Mradi huo unagharimu shilingi milioni 22.5 na unatekelezwa na mkandarasi Negron Builders Company Limited.
Aidha, alisema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Chanika–Kilole DSD yenye urefu wa kilomita 1.7 katika Mji wa Handeni unajengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 1.17. Mwenge wa Uhuru utaweka jiwe la msingi katika mradi huo. Ujenzi wake unatekelezwa na wakandarasi wawili; JP Traders Limited aliyetekeleza kazi yenye thamani ya shilingi milioni 720 na Atimo Construction Limited aliyetekeleza kazi yenye thamani ya shilingi milioni 451.
Aliongeza kuwa miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Mnyongeni katika Wilaya ya Pangani yenye urefu wa kilomita 0.75 kwa kiwango cha lami cha DSD, unaogharimu shilingi milioni 475 na kujengwa na Atimo Construction Co. Limited.
Pia, kuna mradi wa ujenzi wa barabara ya Kange 2 yenye urefu wa kilomita 2.4 kwa kiwango cha lami, unaogharimu shilingi bilioni 1.36 na unatekelezwa na mkandarasi The Globalink General Construction Limited.
Tarimo alisema kuwa mradi mwingine ni ujenzi wa daraja katika barabara ya Bombani–Kiwanda, ambao umefikia hatua ya Box Culvert. Mradi huo unagharimu shilingi milioni 47 na unajengwa na Mwallow Company Limited.
Kwa upande wa Korogwe Mji, alisema kuwa kuna mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami cha DSD wenye urefu wa kilomita 0.65 unaogharimu shilingi milioni 475, ukitekelezwa na RISO Business Holding Co. Limited.
Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa Daraja la Usambara katika barabara ya Vulini–Kirilicha–Kwindoghoi, uliogharimu shilingi milioni 449. Kazi hiyo imekamilika chini ya mkandarasi KIV Company Limited.
Vilevile, kuna mradi wa ujenzi wa barabara ya Shambala–Dochi kwa kiwango cha lami cha DSD, unaogharimu shilingi milioni 993.9 na unatekelezwa na Gloda Construction Limited.
Sambamba na hayo, Tarimo ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga kulinda miundombinu ya barabara kwa kuepuka kutupa taka hovyo na kushirikiana katika kubaini na kutoa taarifa za waharibifu wa miundo mbinu hiyo. mwisho

0 Maoni