NA REBECA DUWE TANGA
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, amewataka wafanyabiashara wote mkoani humo kuhakikisha wanatoa risiti sahihi kwa wateja na kuacha tabia ya kupunguza thamani ya bidhaa au huduma kwenye risiti, akisema kuwa kitendo hicho ni kuiibia Serikali mapato yake.
Balozi Burian alitoa kauli hiyo wakati wa mwendelezo wa maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yaliyoanza Juni 22 mwaka huu, huku kilele chake kikitarajiwa kufanyika Julai 1.
Alisema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa na tabia ya kutoa risiti zenye kiwango cha fedha kisichoendana na thamani halisi ya bidhaa au huduma walizouza, jambo ambalo linaikosesha Serikali mapato ya kodi.
Aidha, alisema miongoni mwa waathirika wakubwa wa tabia hiyo ni wachimbaji wa madini, akiwataka kuwa makini wanapopewa risiti na kuhakikisha kiasi kilichoandikwa kinaendana na fedha walizolipa.
Sambamba na hilo, Balozi Burian aliwataka wananchi wanaoanzisha kampuni binafsi kuhakikisha wanazisajili ndani ya Mkoa wa Tanga na kuzikuza hadi kufikia hadhi ya biashara za kati, hatua ambayo itasaidia kuongeza mapato ya mkoa na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Alisema Mkoa wa Tanga una fursa nyingi za kuongeza mapato kupitia sekta mbalimbali ikiwemo bandari, uvuvi, madini pamoja na biashara za mipakani, hivyo usajili wa kampuni ndani ya mkoa utasaidia kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato yanayojiwekea kila mwaka.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castrol John, alisema TRA ilianzishwa Julai 1, 1996, ikiwa inakusanya takribani shilingi bilioni 531 kwa mwaka, huku kwa mwaka wa fedha 2025/2026 makusanyo yakifikia takribani shilingi trilioni 32.
Alisema mafanikio hayo yamechangiwa na ukuaji wa teknolojia, usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa kodi, utoaji wa elimu kwa walipakodi pamoja na ushirikiano mzuri kati ya TRA na taasisi nyingine za Serikali.
Castrol alisema TRA itaendelea kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari, huku ikiendelea kuboresha mifumo ya teknolojia ya ukusanyaji wa kodi ili kuongeza ufanisi na huduma kwa walipakodi.


