Rebeca Duwe Tanga
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa msaada wa vifaa mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo mkoani Tanga kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye changamoto mbalimbali, wakiwemo watoto njiti, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya mamlaka hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Naibu Kamishna wa Huduma za Kiufundi kutoka Makao Makuu ya TRA, Ted Silkiluwasha, alisema kuwa katika jamii ya Watanzania kuna watu wenye mahitaji maalum wanaohitaji kusaidiwa, hivyo mamlaka imeona umuhimu wa kuwafikia na kuwasaidia.
Alisema Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato ndio unaochangia maendeleo na kuimarisha uwepo wa taifa, hivyo ni muhimu kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika juhudi za maendeleo.
“Sambamba na kuimarisha taifa, hatupendi kumuacha mtu yeyote nyuma. Miaka 30 ya TRA imewezekana kutokana na walipa kodi, na mamlaka inatambua kuwa uhai wa walipa kodi ndio uhai wa TRA. Ndiyo maana tumeamua kutoa msaada huu kwa watoto njiti kama sehemu ya kurudisha kwa jamii inayochangia maendeleo ya taifa kupitia kodi,” alisema Silkiluwasha.
Aliongeza kuwa Julai 1 mwaka huu TRA itatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa na kaulimbiu ya “Tanzania kwa Pamoja Tunajenga Taifa Letu.” Alisema mamlaka imeona umuhimu wa kufika Hospitali ya Rufaa ya Bombo kwa kuwa inahudumia watu wenye mahitaji makubwa, ili kuwajulisha kuwa wao ni sehemu muhimu ya jamii.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John, alisema kuwa mamlaka hiyo inaamini kila Mtanzania ni mlipa kodi wa sasa au wa baadaye, hivyo hata watoto waliotembelewa ni walipa kodi wa kesho na pengine watumishi wa baadaye wa TRA.
Alisema mtazamo huo ndio uliowasukuma kushiriki katika shughuli za kijamii na kusaidia makundi yenye mahitaji maalum.
Aidha, alizitaka taasisi nyingine, hususan mkoani Tanga, kujitokeza kusaidia watu wenye uhitaji na kushiriki katika shughuli za kijamii zinazolenga kuwatia moyo na kuboresha maisha yao.
Naye Nuru Hamisi Omari alisema kuwa hospitali hiyo hupokea watoto njiti kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga. Alieleza kuwa watoto hao hupatiwa huduma mbalimbali ikiwemo kuongeza kiwango cha sukari mwilini na kusaidiwa kupumua kwa kutumia mashine maalum hadi wanapofikia uzito unaoruhusiwa.
Alifafanua kuwa mtoto anaporuhusiwa kwenda nyumbani anatakiwa kuendelea kuhudhuria kliniki maalum ya ufuatiliaji wa ukuaji hadi atakapofikia uzito wa kilo tatu, ndipo huendelea na huduma za kawaida za kliniki.
Kwa upande wake, Muuguzi Kiongozi wa Wodi ya Watoto, Sister Rukia Mbega, ameishukuru TRA kwa kuguswa na mahitaji ya watoto njiti na kutoa msaada utakaosaidia kuboresha huduma kwa watoto hao.
Alisema msaada uliotolewa unajumuisha sabuni, nepi (pampers), dawa na makopo ya maziwa ya unga, vitu ambavyo ni muhimu katika kuwahudumia watoto njiti.




0 Maoni