Tanga: Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdallah, ametangaza rasmi kumpokea aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Tanga Mjini, Rashidi Hamza Jumbe, kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mapokezi hayo yamefanyika mara baada ya kikao cha kikatiba cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Tanga.
Akizungumza mbele ya wanachama wa CCM katika viwanja vya Ofisi za CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu alisema hatua hiyo ni sehemu ya ahadi aliyowahi kutoa alipoteuliwa kuongoza chama hicho mwaka 2022 ya kuhakikisha anakijenga na kukiimarisha CCM mkoani humo.
"Leo nimetimiza ahadi niliyowapa kwamba tutaimarisha chama chetu. Tunawakaribisha viongozi na wanachama wote wanaoamua kujiunga na CCM ili kwa pamoja tuendelee kuitekeleza ilani ya chama na kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan," alisema Rajabu.
Kwa upande wake, Rashidi Hamza Jumbe alisema uamuzi wake wa kuhamia CCM umetokana na utashi wake binafsi, akisisitiza kuwa hakulazimishwa wala kushawishiwa kwa fedha.
"Nimeamua kujiunga na CCM kwa hiari yangu mwenyewe. Niko na akili timamu na niko tayari kukitumikia chama pamoja na kuisemea serikali kutokana na kazi nzuri inayofanya ya kuwaletea wananchi maendeleo," alisema.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika Mkoa wa Tanga na maeneo mengine nchini, ulimfanya kuona umuhimu wa kuunga mkono juhudi za serikali.
"Nimeona maendeleo makubwa yanayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita. Hilo limenifanya niunge mkono juhudi hizo na kushiriki katika kuhamasisha maendeleo kwa wananchi," alisema Rashidi.
Mwisho.

0 Maoni