Mkuu wa Mossad awafuta kazi maafisa waandamizi kwa kushindwa kuipindua serikali ya Iran


Mkuu wa shirika la ujasusi la Israel (Mossad) Roman Gofman amewafuta kazi maafisa wawili waandamizi baada ya mpango wa kuipindua serikali ya Iran kufeli au kutotekelezwa kabisa, kulingana na shirika la habari la Israel Channel 12.

Maafisa hao ni mkuu wa idara ya kukusanya taarifa, aliyeteuliwa miezi michache iliopita, na mkuu wa idara kuhusu Iran, shirika hilo la habari lilisema siku ya Alhamisi. Majina ya maafisa hao hayakubainika.

Channel 12 iliripoti kuwa mpango ulioandaliwa kwa kushirikiana na Marekani ulikuwa na lengo la kuchochea wananchi dhidi ya serikali yao ndani ya Iran, ikiwemo kuunga mkono makundi ya upinzani, huku Israel na Marekani wakifanya mashambulizi ya angani.

Shirika hilo la habari, likinukuu tathmini iliyofanywa, limesema mpango aidha ulifeli au haukufikia hatua ya utekelezaji.

Vyanzo vya kijasusi viliiambia Channel 12 kuwa uhusiano wa wawili hao na Gofman ulitetereka, vikiongeza kuwa kufutwa huko kumekuja huku kukiwa na mabadiliko makubwa katika uongozi wa Mossad pamoja na vipaumbele, hasa kutokana na suala la Iran.

Shirika hilo la habari pia lilieleza kuwa taarifa hizo pia ziliangazia ripoti za kimataifa zikisema kuwa mpango huo ulijumuisha mapendekezo ya kubadilisha uongozi wa Iran na kushirikiana na maafisa wa Marekani kwa mipango ya hatua ya "baada ya serikali" hii.

Ripoti hiyo inasema mpango wa pamoja wa Mossad na CIA ulijumuisha wapiganaji wa Kikurdi kuingia Iran wakisaidiwa na Marekani na Israel na kuweka viongozi wengine katika serikali ya Iran.

Hata hivyo, mipango hiyo ilitibuka mapema, na kusababisha mpango huo kutupwa na wale waliohusika na hilo kuwajibishwa, kulingana na shirika hilo la habari.

Hakukuwa na taarifa yoyote rasmi kutoka kwa Israel kuhusu kufutwa kazi kwa maafisa hao.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikiri Machi 13 kuwa kuipindua serikali ya Iran itakuwa vigumu, akisema kuwa "hakuna uhakika hilo litafanyika."

Marekani na Israel ilianzisha vita dhidi ya Iran Februari 28, na kuwaua watu zaidi ya 3,000. Iran ilishambulia kwa makombora na ndege zisizo na rubani kambi za Marekani katika kanda pamoja na maeneo ya Israel, kuwaua wanajeshi wa pande zote mbili.

Juni 18, Marekani na Iran walitia saini makubaliano na kuanzisha majadiliano ya kufikia mwisho wa mapigano kabla ya kukwama kutokana na kutofautiana kuhusu hakikisho la usalama na uhuru wa kutumia Mlangobahari wa Hormuz

Hali ilikuwa tete tena mwezi uliopita baada ya Marekani kufanya mashambulizi ndani ya Iran, kusababisha Iran kulipa kisasi kote katika kanda, ikiwemo Jordan, Bahrain na Kuwait.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi