Waasi wa Houthi nchini Yemen wamesema wamefanya shambulizi la ndege zisizo na rubani dhidi ya kiwanda cha kusafisha mafuta cha Saudi Arabia, kilichoko katika pwani ya Bahari Nyekundu.
Msemaji wa kijeshi wa kundi hilo, Yahya Saree, amesema shambulizi dhidi ya kiwanda cha Aramco mjini Jazan lilikuwa kulipiza kisasi dhidi ya kile alichokiita uvamizi wa Saudi Arabia kaskazini magharibi mwa Yemen.
Wizara ya Nishati ya Saudi Arabia imesema wazima moto wamefanikiwa kuzima moto uliozuka katika eneo la kiwanda hicho.
Waasi wa Houthi walitangaza mwezi uliopita kuanzishwa kwa kizuizi cha majini dhidi ya Saudi Arabia, hatua iliyochochea tena mzozo kati ya pande hizo na kuongeza shinikizo katika usambazaji wa nishati duniani, ambao tayari umeathiriwa na vita vya Iran.
Wakati huo huo, chombo cha juu cha usalama nchini Iran kimeonya kuwa Mlango wa Hormuz hautafunguliwa hadi Marekani ikubali masharti sita, yakiwemo kulegeza vikwazo dhidi ya Iran, kulipa fidia kwa uharibifu uliosababishwa na vita na kuondoa kizuizi kilichowekwa katika bandari za Iran.
