Kenya: Raia wa Burundi wakimbilia kanisani Mombasa wakihofia usalama wao


Baadhi ya raia wa Burundi wanaofanya biashara ndogo ndogo na kuishi katika jiji la Mombasa Pwani ya Kenya, wamekimblia Kanisani wakihofia maisha yao, baada ya agizo la serikali kuwataka wageni wote wanaoishi na kufanya kazi nchini humo bila vibali kupewa siku 90 kuvitafuta.

Katika mtaa wa Homeboys, eneo la Likoni, Mombasa, kanisa la Beth Even Ministries limekuwa sehemu ya hifadhi ya muda kwa baadhi ya raia wa Burundi ambao wamesitisha biashara zao kufuatia agizo hilo.

Yiatoli Manyilakiza, raia wa Burundi anayejipatia kipato kwa kuuza mayai, ni miongoni mwa walioathirika.

“Nafanya kazi ya kuzungusha mayai, rais wa Kenya amesema twende kwetu! Hakuna nauli ya kwenda na nataka kurudi nyumbani.”

Kwa baadhi ya wanawake na watoto, changamoto kubwa sasa ni namna ya kuendelea kujikimu.

“Nimelia nikisema sasa mimi watoto wangu vipi? Tutafika huko Burundi vipi na vitu tulikuwa tumepanga huku. Tunaenda bila chochote hatuna pesa za kutumia njiani.”

Celestine Shimirimana, mhubiri na mmiliki wa mgahawa huko Likoni, anasema kusitishwa kwa biashara hizo kunaathiri pia uchumi wa eneo hilo.

“Mtu akikuambia funga kazi ni ishara tosha kukuambia sikutaki. ”

Mchambuzi wa masuala ya kijamii na kiuchumi eneo la Pwani, Shaaban Mwalimu, anasema utekelezaji wa hatua hizo unapaswa kuzingatia pia malengo ya ujumuishaji wa kikanda.

“Kenya hapa kuna matatizo mengi ya kiuchumi, kuna gharama ya maisha ziko juu, haya maswala yalikuwa yashughulukiwe. Je? Ni nani sasa anayesababisha gharama ya maisha kuwa juu hapa ni wageni au ni sera ambazo labda serikali inazichukua.”

Kwa sasa, baadhi ya raia wa Burundi walioathirika wanasubiri hatua zaidi kutoka kwa mamlaka za Kenya, kuhusu hatma yao.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi