Na Rebeca Duwe, Tanga
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) Mkoa wa Tanga limejipanga kukabiliana na ongezeko la watu linaloendelea kujitokeza mkoani humo kwa kuongeza ujenzi wa nyumba za makazi na biashara.
Hatua hiyo inatajwa kuwa muhimu kutokana na kasi ya ukuaji wa mji wa Tanga pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi, ikiwamo shughuli zinazohusiana na Bandari ya Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Meneja wa NHC Mkoa wa Tanga, Mhandisi Musa Kamendu, alisema shirika hilo limeanza kutekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha linakidhi mahitaji ya nyumba kwa wakazi wa mkoa huo.
Kamendu alisema mikakati hiyo inahusisha ujenzi wa nyumba mpya pamoja na ukarabati wa nyumba chakavu zinazomilikiwa na shirika hilo.
«“Sisi kama Shirika la Nyumba kazi yetu ni kujenga nyumba bora. Hivyo, ili kukabiliana na ongezeko la wakazi, tuna miradi mbalimbali inayolenga kujenga nyumba za makazi na biashara, ikiwamo mradi wa Mkwakwani ambao tayari unaendelea kwa ajili ya kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba,” alisema Kamendu.»
Nyumba 20 kujengwa
Kwa mujibu wa Kamendu, kwa sasa NHC inaendelea na ujenzi wa nyumba 20 za makazi, ambazo ni sehemu ya juhudi za kuongeza idadi ya nyumba na kukabiliana na mahitaji yanayotokana na ongezeko la watu.
Alisema ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Tanga, ikiwamo kuongezeka kwa shughuli katika Bandari ya Tanga, umechangia ongezeko la watu na mahitaji ya huduma mbalimbali, likiwamo suala la makazi.
“Uchumi wa mkoa unakua kutokana na shughuli mbalimbali, ikiwamo Bandari ya Tanga kukua na kuanza kushusha meli kubwa za mizigo. Hivyo, ongezeko la shughuli za kiuchumi linaendana pia na ongezeko la watu,” alisema.
Sekta binafsi nayo yashiriki
Kamendu alisema ongezeko la watu na mahitaji ya nyumba limeifanya pia sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika ujenzi wa nyumba za makazi na biashara.
Alisema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kusaidia Serikali kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa makazi, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji katika kuleta maendeleo.
Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji ili kuongeza shughuli za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya Mkoa wa Tanga na taifa kwa ujumla.
Kwa kasi ya ukuaji wa mji wa Tanga na ongezeko la shughuli za kiuchumi, ujenzi wa nyumba mpya unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kukidhi mahitaji ya wakazi na wawekezaji wanaoendelea kuingia mkoani humo.
