Apr 23, 2021

Waziri Bashungwa akutana na Balozi wa China nchini

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China kwa lengo la kuboresha  ushirikiano kwenye Sekta  zilizo chini ya Wizara hiyo.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Aprili 22, 2021 katika Ofisi za TBC Jijini Dodoma ambapo wamegusia mambo kadhaa ya kuendeleza Wizara na taasisi zake kimkakati ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi, teknolojia na uchumi duniani.

 Waziri Bashungwa alimshukuru Mhe.Balozi kwa Jitihada walizozifanya kujenga Uwanja wa Taifa uliopewa jina la Uwanja wa Benjamin Mkapa na kumuomba Balozi kujenga Uwanja mwingine mkubwa Kanda ya Ziwa ili kumuenzi Hayati John Pombe Magufuli.

Kuhusiana na Tasnia ya Filamu nchini, Waziri Bashungwa amemuomba Mhe. Balozi  kuweza kusaidia kujenga maktaba ya vifaa vya filamu nchini ambayo itakuwa katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo.

Amesema, maktaba hiyo itawasaidia wazalishaji Filamu nchini kuwa na kuweza kuazima na kurudisha vifaa tofauti na sasa ambapo kila mmoja anahangaika kutafuta vifaa peke yake na kwa gharama kubwa.

Pia alimuomba Mhe. Balozi  kuutangaza Utamaduni wa Tanzania nchini mwao na sehemu mbalimbali duniani kwa kuwa   nchi ya China imepiga hatua kubwa kwenye eneo la sayansi na teknolojia.


Kwa upande wake,  Balozi wa China nchini Mhe Wang Ke amempongeza Waziri Bashungwa kwa Kuteuliwa tena na kuaminiwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpa nafasi ya kuongoza tena Wizara hiyo na kuahidi kushirikiana naye.

Mhe. Balozi Wang ameahidi kufanyia kazi maombi yote aliyotoa Mhe. Bashungwa ambapo amesema  atajadiliana  na Serikali yake ili kuona ni kwa namna gani wanaweza kushughulikia maombi hayo.

Balozi Wang amemuomba Waziri Bashungwa kuweka karibu ushirikiano wa TBC na Kampuni ya Star Times nchini ili kuweza kuimarisha Sekta ya Habari hapa nchini.

Ameipongeza Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi  iliyoiunga mkono nchi ya China katika kuandaa Michuano ya Olimpiki 2008.

Balozi Wang ametoa fursa za nafasi za mafunzo kwa  watumishi wa Serikali nchini China ili kuweza kuongeza ujuzi wa kuhabarisha jamii kiujumla.

Tanzania imekuwa na  ushirikiano wa karibu na wa muda mrefu  na nchi ya China ambao umekuwa wa kihistoria tangu kipindi cha uhuru wake chini ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

 

Share:

Wabunge wahimizwa kuwasilisha kero na malalamiko yanayohusu Utumishi wa Umma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewahimiza Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha kero na malalamiko ya kiutumishi yaliyo katika majimbo yao ili ofisi yake iweze kuyafanyia kazi.

Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2021/22 ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ili Bunge liweze kujadili na kuidhinisha.  

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, amedhamiria kuingoza ofisi yake kupunguza au kuyamaliza kabisa malalamiko ya Watumishi wa Umma na wananchi yanayohusu masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Akihimiza ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi, amewaelekeza Waajiri wote, hasa Maafisa Utumishi kuwasilisha madai ya watumishi kwa wakati ili kupunguza mlundikano wa madeni ya watumishi yanayotokana stahili zao.

Ameongeza kuwa, Ofisi yake itaimarisha matumizi ya mfumo wa kushughulikia malalamiko katika Taasisi za Umma ili malalamiko ya watumishi na wananchi yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati.

Mhe. Mchengerwa ametoa rai kwa Maafisa Utumishi kushughulikia changamoto za Watumishi wa Umma kwa wakati ili kujenga ari na morali ya watumishi wa umma kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Mwajiri na Afisa Utumishi yeyote atakayeshindwa kutatua kero na malalamiko yaliyo ndani ya uwezo wake, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake”, amesisitiza Mhe. Mchengerwa.  


Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya kamati yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole ameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma ili kuwajengea hali kiutendaji.

Aidha, Mhe. Polepole ameliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya shilingi 727,932,861,000/= kwa ajili utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na taasisi zilizo chini yake.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litajadili ili kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2021/22 ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora yaliyowasilishwa Bungeni na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.

 

Share:

Ujumbe wa ubaguzi uliotumwa na afisa wa polisi Ufaransa wafichuka

Imebainishwa kwamba kulikuwa na ujumbe wa kibaguzi kwenye simu ya mmoja wa maafisa wa polisi watatu ambao walituhumiwa kwa kumpiga mwanamuziki wa Kiafrika nchini Ufaransa.

Katika kipindi kimoja cha kituo cha runinga ya France 2, zilionyeshwa kanda kadhaa za simu za mmoja wa maafisa watatu wa polisi wanaotuhumiwa kwa kumpiga mwanamuziki wa Kiafrika mnamo Novemba 21 mwaka jana.

Ujumbe uliotumwa mwezi Mei katika kikundi cha mazungumzo ya polisi unaonyesha picha ya afisa wa polisi wa Marekani Derek Chauvin akimshinikiza Mwafrika-Mmarekani George Floyd shingoni mwake kwa goti. Kwenye picha, imeandikwa, "Wakati wa kuvuta hewa ya mara ya mwisho usiku kutoka kitandani."

Mnamo mwezi Agosti, polisi walituma ujumbe wa matusi kwa jamaa wa karibu wa mhathiriwa mwenye asili ya Kiafrika ambaye alikuwa akiuliza juu ya kesi hiyo. Baada ya jamaa yake kumuonya asijihusishe na ubaguzi wa rangi, polisi walidai kwamba haukuwa ubaguzi.

Katika mtaa wa 17 wa Paris, mtayarishaji wa muziki Michel Zecler alikabiliwa na vurugu za maafisa 3 wa polisi, wawili wao wakiwa wamevalia sare, ambao walikuja nyuma yake alipoingia studio yake. Baada ya wito wa msaada kutoka kwa Zecler ambaye alipigwa na polisi kwa dakika 20, majirani zake walikwenda kumsaidia kutoka kwa mlango wa nyuma wa ofisi.

Kwa kuona majirani zake, polisi walimwacha Zecler na kuondoka studio na kuita timu ya kuimarisha usalama.  Afisa wa polisi alikuwa amerusha mtungi wa gesi ya kutoa machozi ndani, na kusababisha Zecler kutoka nje.

 

Share:

Rais Samia Suluhu afanya uteuzi wa Viongozi 4


 Rais Samia Suluhu afanya uteuzi wa Viongozi 4


Share:

MAGAZETI YA LEO 23/4/2021


 Share:

Apr 22, 2021

Njia rahisi ya kutengeneza chakula cha samaki

Mfugaji anaweza kupunguza gaharama za kununua chakula kwa ajili ya samaki, kwa kutengeneza chakula mwenyewe kwa kutumia malighafi ulizo nazo katika eneo lako. Tumia resheni rahisi ambayo itakupatia chakula cha kutosha na kwa gharama nafuu.

Mahitaji

 • Pumba ya mahindi sadolini 1.
 • Pumba ya ngano au mpunga sadolini 1.
 • Dagaa sadolini 1.
 • Kilo moja ya soya.
 • Robo kilo ya mashudu ya pamba au alizeti.
 • Namna ya kuandaa

  • Changanya malighafi hizo kwa pamoja.
  • Saga hadi zilainike.
  • Kanda kama vile unga wa kutengenezea chapati.
  • Weka kwenye mashine ya kusaga nyama au kutengenezea tambi.
  • Anika kwenye jua la wastani.
  • Baada ya kukauka, vunja vunja kwenye vipande vidogo vidogo hasa kwa kuzingatia umri wa samaki unaokusudia kuwalisha.
  • Tumia lishe hiyo kwa samaki mara tatu kwa siku.
Share:

Fahamu kuhusu ugonjwa wa Polio kiundani zaidi

Polio ni ugonjwa wa kuambukiza usababishwao na virusi, huathiri neva na kusababisha ulemavu.

Kutokana na taarifa za shirika la afya duniani:
Polio huathiri zaidi watoto wa umri wa chini ya miaka mitano
Ulemavu hutokea kwa mmoja kati ya maambukizi 200
Mpaka 2013 ni nchi tatu ambazo bado kuna mlipuko wa ugonjwa huu wa kupooza Afghanistan, Pakistan na Nigeria. Ila kutokana na Taarifa kutoka wizara ya afya ya Tanzania ilipokea taarifa kutoka shirika la afya duniani kuwa kuna mlipuko katika nji jirani ya Kenya, wilaya ya Fafi.

Je ni zipi dalili za ugonjwa huu?
Dalili hizi hudumu kwa kati ya siku 1 hadi 10
Homa
Maumivu ya kichwa
Kutapika
Uchovu
Maumivu ya shingo
Maumivu ya mgongo
Maumivu ya mikono na miguu
Misuli kukakamaa

Je ni matatizo gani mtu huweza kupata baada ya maambukizi haya?
Kupooza misuli
Ulemavu wa miguu

Vipimo:
Virusi vya polio huweza kuonekana katika makohozi, kinyesi na maji maji ya uti wa mgongo.

Matibabu
Hamna matibabu ya maambukizi haya, kwahiyo ni tiba ya dalili ambayo hutolewa:
Kupumzika
Dawa za kutuliza maumivu na kushusha homa
Antibiotiki kuzuia maambukizi nyemelezi
Mazoezi kiasi kwaajili ya kuzuia kukakamaa
Na kula chakula bora

Kinga
Ni chanjo ya Polio ambayo hutolewa pamoja na chanjo nyingine kwa watoto baada tu ya kuzaliwa, na kurudiwa tena katika wiki ya nne, ya nane na mwisho ya kumi na mbili.

Share:

Mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuanzisha Biashara


Yawezekanan kwa muda mrefu umekuwa ukitaabika namna gani unaweza kuanzisha biashara na si biashara tu bali biashara yenye kukuletea mafanikio, yafutayo ndiyo mambo ya muhimu ya kuzingatia ili kuanzisha biashara yenye mafanikio.

Wazo
Katika kila wazo zuri la biashara ulilo nalo kuna mamia ya watu wana wazo hilohilo. Jambo muhimu la kuzingatia ni kama wazo lako lipo, au je kuna watu tayari  wanafanyia kazi wazo lako? Kama jibu ni ndio jiulize je,unaweza kupata wazo jingine au kufanya biashara hiyohiyo kwa kujitofautisha na watangulizi wako?

Jiulize maswali yafuatayo: Je,kuna mpango mzuri wa biashara? Je watu wengine wanaofanya biashara hiyohiyo wanatengeneza hela? Kama wanapata nini nifanye ili nifanikiwe na niingize hela zaidi yao?. Mwisho unahitaji kujua kama wazo lako kisheria linakubalika au la!

Mpango wa biashara
Tengeneza mpango wa biahara . Watu wengi huwa wanaruka kipengele hiki na kuanza moja kwa moja biashara na hatimae biashara zao huishia njiani. Kutengeneza mpango wako utakusaidia kulinda mtazamo wako na mwelekeo wako kibiashara. Fikiria mpango wa biashara yako kama kitu muhimu sana. Huwezi kuanza kujenga nyumba bila ramani.

Upekee wa biashara
Amua biashara yako isimame kwa namna gani,lazima uwe na ushindani kwenye biashara yako utakao kutofautisha wewe na washindani wako.Ipe thamani biashara yako.

Nani yuko kwenye gari lako
Tambua kwamba wewe ndo dereva na gari ni kampuni au biashara yako na bado limesimama au halijaanza safari. Amua unaenda wapi? Amua unaenda na akina nani? Amua unataka kufika wapi?

Utaendesha biashara peke yako au unahaji watu wa kuajiri?

Umuhimu wa mteja.
Soko lako kuu ni lipi? Kabla ya kupanga mbinu za kuuza unahitaji kujua soko lako lengwa ni lipi? Soko lengwa ni kikundi cha watu ambacho kampuni yako imetengeza bidhaa kwa ajili yake.

Tengeneza tovuti kwa ajili yab biashara yako.
Tengeneza tovuti au blogu maarumu kwa ajili ya biashara yako. Haijalishi utakuwa unatengeneza matofali au utakuwa ukilima kuwa na  tovuti au blogu ni muhimu sana. Blogu yako itakuweka mbele kuweza kuuza biashara yako mtandaoni. Ni muhimu pia wewe  kuwa na email kwa ajili ya biashara yako.

Muonekano wako wa kwanza (first impression)
Una mbinu gani ya kwenda sokoni? Utawezaje kuwashawishi watu? Elewa mambo gani ni muhimu ili kuliteka soko? Kuelewa mbinu gani ni muhimu sana hasa pale watu wanapokuwa hawajui kama bidhaa yako ipo? Wapi inapatikana? Na namna ya kuinunua?

Fahamu jinsi ya kuipiga tafu biashara.
Je hela ya kuanzisha na kuendesha biashara itatoka wapi?Hili linaweza kuwa jambo ambalo linasumbua ila fuatilia kujua wengine waliwezaje kufanya biashara zao. Je, utalipwaje? Kama ni tigo pesa mpesa au keshi ya mkononi.

Je una elimu ya kutosha?
Kitu cha kwanza tunasikia kutoka kwa wafanya biashara wanasema ningelijua.hii inaonesha wazi huyu mtu hakufuatilia kwa umakini biashara yake kabla ya kuianza. Jiandae kukabiliana na changamoto yoyote itakayojitokeza na kuifanyia kazi.

Jifunze mambo yahusuyo biashara.
Ni muhimu sana kufuatilia biashara yako kwa kusoma makala na vitabu mbalimbali vinavyohusu biashara hiyo. Hii itakujengea msingi mzuri katika biashara lakini pia utaweza kujua mabadiliko makubwa yanayotokea kwenye biashara usiku na mchana.

Hivyo nasisitiza tena endelea kusoma kila siku ili ujue ni mabadiliko gani yanatokea kwenye biashara yako.
Share:

Jinsi ya kusafisha kucha zako za miguuni au mikononi

Inashauriwa kwamba kabla ya kuchukua uamuzi wa kwenda kununua vifaa husika ambavyo utavitumia unapaswa kufahamu aina ya kucha ili uweze kununua vifaa vinavyoendana na kucha zako kwa lengo la kuzilinda badala ya kuvamia na kuziharibu.

Kwa kawaida kucha za mikononi na miguuni zinakabiliwa na mazingira magumu kutokana na majukumu ya kazi za kila siku hali inayochangia kuziweka katika mazingira magumu kiafya.

Mbali na kucha kukosa afya, pia kuharibu shepu yake ya awali kutokana na shughuli za kila siku katika maisha ya binadamu yeyote, hivyo ni vyema kuzikinga kucha zako na maradhi kwa kuzifanyia usafi kila siku au mara kadhaa kwa wiki ili kuzilinda zaidi.

Ili kuweza kugundua aina ya kucha zako katika kuzipangilia wakati wa kuzifanyia usafi, unapaswa kuwa makini wakati unachagua rangi ya kupaka, kuangalia muonekano wa kucha zako zilivyo ili uweze kupangalia rangi ziweze kuwa na mvuto zaidi.

Ni vyema kwa mtu anayejali afya ya kucha zake kuchukua muda mwingi kufuatilia kucha zake na kuelekeza nguvu zake katika kuhakikisha zinakuwa katika matunzo mazuri na kujitahidi kubuni mtindo ambao unaweza kuwa tofauti na wengine ambao wanapenda kuzifanya kawaida.

Hata hivyo katika kutunza kucha ziwe nzuri, vyakula ambavyo ni mlo kamili ni muhimu sana, vinginevyo utajikuta ukishauriwa na wataalamu kutumia vitamini mbalimbali kama vile vitamini A, vitamini C, Culcium, Folic Asidi, Protini na Vitamini B12.

Jinsi ya kusafisha kucha zako.
Tafuta vifaa vizuri vya kisasa vya kutunzia kucha.
Tumia brush ya kucha kwa kusugua chini ya kucha na kuutoa uchafu na kufikia sehemu ngumu ambapo uchafu unajilundika. Unaweza tumia mswaki ukiwa huna vifaa vya kisasa.     
                                                                                   
Tumia maji moto na sabuni ya kunawia mikono. 
Anza kwa kusugua chini kabisa kwa kushikilia brush chini na sugua kuanzia nyuma kuja mbele pole pole, kisha juu ya kucha fanya hivyo kwa kuzunguka.

Toa rangi kwa kuloweka pamba kwenye polish remover na usugue kwa vidole vyenye hinna huna haja ya kuitoa. Kwa vidole vya afya na nguvu vipumzishe kwa kutumia polish kila baada ya wiki kadhaa.
       
Loweka kucha na maji kwenye bakuli,au sinki,au kifaa cha uwezo wako hata dishi poa, kwa maji ya moto ya uvuguvugu na pitisha sabuni ya kunawia mikono. Na ni kucha tu usiloweke mkono mzima kwa dakika tatu, sabuni kwenye maji hufanya mikono kuwa mikavu .

Suuza kwa maji ya bomba ya uvuguvugu, au yalokua kwenye chombo yaani jimwagie, kisha zifute na taulo laini. Kisha tumia kikatio kucha kukata maana zitakua laini,au kifaa cha kuzipunguza kuweka sawa kama hauzikati.
Share:

Papa aahidi kuizuru Lebanon, atoa wito wa kutatua mkwamo wa kisiasa


Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis, amemuahidi waziri mkuu mteule wa Lebanon Saad al-Hariri leo, kuwa ataitembelea nchi hiyo lakini baada tu ya pande za kisiasa kuweka kando tofauti zao kwa manufaa ya watu. 

Vatican imesema Hariri, ambaye pia atakutana na viongozi wa Italia wakati wa ziara yake fupi, alifanya mazungumzo na papa kwa takribani dakika 30. 

Hariri aliiambia televisheni ya Labanon baadae kwamba papa atazuru ikiwa tu wanasiasa wa taifa hilo lililogawika, wataweza kukubaliana kuhusu serikali mpya.

 Taarifa ya Vatican ilisema Francis alikariri ukaribu wake na watu wa Lebanon, wanaoishi katika nyakati ngumu na za mashaka, na kuzungumzia wajibu wa makundi yote ya kisiasa kutaguliza mbele maslahi ya taifa hilo.

Share:

Biden afungua mkutano wa dunia wa tabianchi kwa ahali ya kupunguza gesi chafu


Rais Joe Biden ameahidi kupunguza kwa nusu viwango vya utoaji wa gesi ya ukaa nchini Marekani, kufikia mwishoni mwa muongo huu, wakati akifungua mkutano wa kilele wa mtandaoni uliohudhuriwa na viongozi 40 wa dunia kuhusu mabadiliko ya tabianchi. 

"Tunajua umuhimu wa hili, kwa sababu wanasayansi wanatuambia kwamba huu ni muongo wa maamuzi. Huu ndiyo muongo ambamo tunapaswa kufanya maamuzi yatakayoepusha madhara mabaya zaidi ya mzozo wa tabianchi," alisema Biden. 

Mkutano huo wa siku mbili unalenga kuyahamasisha mataifa yenye uchumi mkubwa kuweka malengo makubwa zaidi ya kupunguza viwango vya gesi ya kaboni, na unatazamwa kama maandalizi muhimu kuelekea mkutano wa mazingira wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mjini Glasgow, Scotland, mwezi Novemba.

Share:

Azam yabanwa mbavu na Dodoma


Klabu ya Azam FC imetoshana nguvu na Dododma jiji FC kwa kutoka sare ya mabao 2-2, katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara uliochezwa katika dimba la Jamuhuri Dododma.

Azam FC ndio walikwa wa kwanza kufunga bao kupitia kwa Prince Dube dakika ya pili ya mchezo, lakini baadae kipindi cha pili dakika ya 71 Seif Karihe akaisawazishia Dodoma Jijiji na dakika 6 baadae Anuary Jabir akafunga tena bao la pili na kuipa uongozi Dodoma mpaka dakika ya 90 ambapo Azam FC wakasawazisha kupitia kwa Obrey Chirwa.

Kwa ushindi huu Azam wanasalia nafasi ya tatu wakiwa na alama 51, wakatia Dodoma wanafikisha alama 38 wakiwa nafasi ya 6 kwenye msimamo wa ligi.

ukiachana na mchezo huo, Mchezo wa mapema leo ulichezwa Saa 8:00 mchana ambapo Ihefu FC walikuwa wenyeji wa Tanzania Prisons, na wenyeji wakafanikiwa kuondoka na alama zote tatu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, bao la pekee katika mchezo huo limefungwa na Raphael Daud dakika ya 6.

Ihefu imepanda kwa nafasi moja kutoka ya 17 hadi 16 wakifikisha alama 27, na Tanznaia Prisons wameshuka kwenye msimamo kutoka nafasi ya 8 mpaka ya 9 wakisalia na alama 34.

Share:

Manowari ya Indonesia yapoteza mawasiliano


Manowari ya KRI Nanggala-402 inayomilikiwa na kikosi cha Indonesia, na ambayo ina wafanyikazi 53, iliripotiwa kukapoteza mawasiliano na kituo cha udhibiti.

Iliarifiwa kuwa manowari hiyo ilikuwa karibu na pwani ya kaskazini ya kisiwa cha Bali kwa ajili ya zoezi la kijeshi.

Akizungumza na shirika la habari la Uingereza la Reuters, afisa mmoja wa jeshi aliripoti kwamba Australia na Singapore ziliombwa msaada kwa ajili ya shughuli ya uokoaji.

Hakuna jibu lolote lililotolewa kutoka kwa nchi hizi mbili kufuatia wito wa msaada.

Manowari ya KRI Nanggala-402, yenye uzito wa tani 1,395, ilitengenezwa nchini Ujerumani mnamo mwaka 1978 na ilikuwa imepitia kipindi cha miaka miwili ya ukarabati mnamo mwaka 2012.

Share:

Uingereza yaomba msamaha kwa kushindwa kuwakumbuka wanajeshi weusi waliofarika wakati wa vita vya dunia


Serikali ya Uingereza imeomba msamaha kwa kufeli kuwaweka katika kumbukumbu wanajeshi weusi na wale wa kutoka bara Asia waliofariki wakipigania ufalme wa Uingereza.

Ripoti moja ya tume ya makaburi ya jumuiya ya madola ilibaini kwamba hatua hiyo ilitokana na ubaguzi.

Baadhi ya wanajeshi walikumbukwa kwa pamoja ama majina yao yalisajiliwa huku wenzao wazungu waliwekewa mawe katika makaburi yao.

Katika bunge la Uingereza waziri wa ulinzi Ben Wallace alionesha kujuta. Aliambia wabunge hakuna wasiwasi ubaguzi ulifanyika baada ya vita ya kwanza ya dunia.

Tume ya makaburi ya jumuiya ya madola pia iliomba msamaha kuhusu matokeo ya ripoti hiyo. Mbunge kutoka chama cha Leba David Lammy ambaye alikuwa kiungo muhimu katika kulianzisha suala hilo alilitaja kama 'wakati muhimu'.

Bwana Wallace alisema: Kwa niaba ya Tume ya makaburi ya jumuiya ya madola na serikali wakati huo na sasa, nataka kuomba msamaha kwa kufeli kuafikia matarajio yetu miaka yote hiyo na kuonesha kujuta kwamba imechukua muda mrefu ili kubadilisha hali hiyo. Huku tukiwa hatuwezi kubadili yaliopita, tunaweza kufanya mabadiliko na kuchukua hatua, alisema.

Uchunguzi ulianzishwa kufuatia Makala ya 2019 yaliowasilishwa na bwana lammy , kwa jina unremembered

Ulibaini kwamba takriban wanajeshi 116,000 waliofariki katika vita ya kwanza ya duniani , wengi wao wakiwa Waafrika , Wahindi ama watu waliotoka Misri , hawakukumbukwa hata kidogo''.

Pia ilibaini matamshi ya kibaguzi kama vile yale yaliotolewa na gavana mmoja wa ukoloni wa Uingereza 1923 kwamba: Watu hao wasingeweza kuelewa ama kuthamini umuhimu wa jiwe katika kaburi.."

Katika mahojiano na BBC , waziri kivuli wa haki Bwana Lammy alisema kwamba huku wakitengeneza makala hayo nchini Kenya na Tanzania , aligundua makaburi ya pamoja ambapo Waafrika walizikwa bila utambuzi wowote ule''.

Alisema kwamba ni makosa kwamba wanaume waliohudumia ufalme wa Uingereza hawakukumbukwa vyema , lakini akaunga mkono ripoti hiyo.

''Nafurahia kwamba heshima ambayo watu hawa walihitaji , baada ya kuchukuliwa kutoka katika vijiji vyao na kulazimishwa kufanyia kazi ufalme wa Uingereza na kwamba heshima waliohitaji kupewa katika kifo wanapatiwa bila kusita'', alisema.

Bwana lammy aliongezea kwamba kazi inapaswa kufanywa ili kupata majina yao katika kumbukumbu iwapo hilo litahitajika na kubaini jinsi jamii zao zinataka wakumbukwe.

Mwanahistoria Prof David Olusoga, ambaye runinga yake ilionesha unremembered, alisema kwamba tume hiyo ilijua kuhusu suala hilo na ikalazimishwa kukiri historia yake. ".

Aliambia BBC kwamba msamaha hautoshi na kwamba raslimali zitahitajika kufanya kazi iwapo tume hiyo ilikuwa tayari kulipa haki.

''Iwapo tume ya makaburi ya jumuiya ya madola iliunda kamati na kugundua kwamba wanajeshi 100,000 wa Uingereza walizikwa katika makaburi ya pamoja ambayo hayajatambuliwa na Makala hayo kuthibtisha kwamba hilo lilifanyika makusudi , je ni nini watakifanya''? aliuliza.

"Wanahitaji kupatiwa haki yao kama ile ya wale wengine na wanahitaji haki hiyo sasa hivi.

Wanajeshi wapatao milioni sita kutoka kwa ufalme wa Uingereza walihudumu katika vita ya kwanza ya dunia.

Kati ya wanajeshi 45,000 na 54,000 kutoka bara Asia na barani Afrika waliofariki katika vita hivyo walitambuliwa bila kuwepo kwa usawa, tume hiyo ilisema.

Share:

Kituo cha afya Makambako chawatoza shilingi 4000 watoto chini ya miaka 5 ili kumuona daktari


Brigither Nyoni na Amiri Kilagalila,Njombe

Wananchi mjini Makambako wameiomba serikali kutoa  ufafanuzi kuhusiana na  mabadiliko ya utoaji wa huduma za afya katika kituo cha afya Makambako baada ya watoto chini ya miaka mitano kutakiwa kulipia fedha ili waweze kupatiwa matibabu.

Wakizungumza na mwandishi wetu baadhi ya wanawake mjini Makambako  wamesema kuwa awali watoto wenye umri chini ya miaka mitano walikuwa wanatibiwa bure lakini kwa sasa wanaambiwa walipe elfu nne ili wapatiwe huduma.

Akizungumza kwa niaba ya mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, FROLA MDUGO amekiri kutokea kwa mabadiliko hayo na kueleza kuwa kwa sasa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanatakiwa kulipia elfu nne ambayo ni Kwa ajili ya kumuona daktari  lakini upande wa vipimo na dawa watapatiwa bure.

Hata hivyo amesema kuwa kwa wanawake wajawazito kwa sasa watapatiwa matibabu bure endapo watakuwa na tatizo la afya linalohusiana na ujauzito lakini kama watakuwa na tatizo la kiafya ambalo halihusiani na ujauzito wanatakiwa kulipia matibabu yote.

Sera ya Afya nchini Tanzania  inataka huduma za Afya kwa wazee, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupata bure, lakini kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya makundi hayo  kutokana na kutozwa fedha za matibabu.

Share:

Kombora la kutungua ndege la Syria laanguka karibu na kinu cha nyuklia cha Israel


Kombora moja la kuangusha ndege la Syria limelipuka kusini mwa Israel , takriban kilomita 30 kutoka kinu kimoja cha siri cha kutengeneza nyuklia .

Ving'ora vilisikika kabla ya mlipuko huo mkubwa kusikika katika eneo la Dimona. Hakuna majeraha au uharibifu ulioripotiwa.

Jeshi la Israel limesema kwamba kombora hilo ni mojawapo ya makombora kadhaa ambayo yalirushwa kulenga silaha moja ya kutungua ndege.

Silah hiyo ilijibu kwa kushambulia silaha za kulinda anga ya taifa hilo.

Jeshi la Syria lilisema kwamba makombora ya Israel yalilenga maeneo karibu na mji mkuu wa Damascus.

Iran kulipiza kisasi shambulio dhidi ya mtambo wake wa nyuklia

''Baadhi ya makombora yalitunguliwa na kuangushwa , lakini wanajeshi wanne wa Syria walijeruhiwa na kuna baadhi ya maeneo yalioharibiwa'', liliongezea

Shirika la haki za kibinadamu nchini Syria The Syrian Observatory for Human Rights, lenye makao yake Uingereza liliripoti kwamba makombora ya Israel yalishambulia kambi za kulinda anga ya taifa hilo katika mji wa Dumayr, takriban kilomita 40 kaskazini mashariki mwa Damascus.

Eneo hilo linaaminika kuwa lenye makombora ya Iran yanayomilikiwa na wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran pamoja na jeshi la Syria katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Hivi majuzi , iliripotiwa kwamba usalama wa maeneo ya Dimona na bandari ya Eilat nchini Israel ulikuwa umeimarishwa iwapo kungetokea mashambulizi yanayotekelezwa na vikosi vinavyoungwa mkono na Iran katika eneo hilo ikiwemo vile vilivyomo nchini Syria.

Hali ya wasiwasi inaendelea kutanda kati ya maadui hao wawili huku Iran ikilaumu Israel kwa kutekeleza kitendo cha hujuma dhidi ya kinu chake cha kuzalisha madini ya Uranium cha Natanz mapema mwezi huu.

Israel haikusema kwamba ilihusika na shambulio hilo.

Kinu cha nyuklia cha Israel kilichopo Dimona kinadaiwa kutengeneza silaha.

Israel haijathibitisha au kukana kwamba inamiliki silaha za kinyuklia chini ya sera yake yenye utata.

Share:

Ashtakiwa kwa 'kumuua na kumla mama yake'


Mtu mmoja ameshtakiwa nchini Uhispania kwa tuhuma za kumuua mamake, kisha kuukata vipande mwili wake na kuula.

Alberto Sanchez Gomez alikamatwa mwaka 2019 baada ya maafisa wa polisi kwenda katika nyumba ya mamake mwenye umri wa miaka 66 kutokana na wasiwasi wa rafiki mmoja.

Maafisa wa polisi wanasema kwamba walipata vipande vya mwili vilivyotapakaa ndani ya nyumba hiyo, huku vingine vikiwa vimehifadhiwa katika ndoo ya plastiki.

Mshukiwa ameambia mahakama kwamba hakumbuki kuukatakata mwili na kumla mamake.

Amedaiwa kuugua tatizo la kiakili pamoja na tumiaji wa mihadarati kabla ya kukamatwa kwake.

Vyombo vya habari vya Uhispania vinasema kwamba bwana huyo alikuwa nafahamika na maafisa wa polisi kwa kumfanyia ghasia mamake , Maria Soledad Gomez, mara kwa mara na kwamba alikiuka agizo la mahakama la kukaa mbali na mzazi wake huyo wakati wa kukamatwa kwake.

Mahakama ilielezewa kuhusu tukio ambalo maafisa wa polisi walikutana nalo katika nyumba hiyo mashariki mwa Madrid mnamo Februari 2019.

Baadhi ya mabaki yake yalikuwa katika hali ya kutaka kupikwa na mengine kuhifadhiwa, linaripoti gazeti la El Mundo.

Mshukiwa aliyekuwa na umri wa miaka 26 wakati huo, alikiri kumnyonga mamake na kusema kwamba mara nyengine alikula vipande vya mwili huo na mara nyenagine akawapatia mbwa.

Share:

Wanawake na watoto wawekwa kizuizini zaidi ya masaa 9 kwa kukosa mchango wa shule


Na Amiri Kilagalila,Njombe

Wananchi wa kijiji cha luduga kilichopo wilaya ya wanging'ombe mkoani Njombe wamelalamikia kitendo cha viongozi wa kijiji hicho kuwakamata na kuwaweka ndani ya ofisi kina mama wakiwa na watoto wadogo kwa tuhuma za kutolipa mchango wa ujenzi wa shule ya sekondari. 

Wakizungumza na mwandishi wetu baadhi ya wananchi hao wamesema kuwa licha ya kuwa na matatizo ya kiafya na kuwa na watoto wadogo bado viongozi hao wamewakamata na kuwafunga kwa zaidi ya saa 9.

Akizungumzia kuhusiana na malalamiko hayo mwenyekiti wa kijiji hicho  AMADY OMARY MPANYE  amekiri kuwepo kwa zoezi hilo la kuwakamata wale wote ambao hawajalipa mchango na kueleza kuwa hajapokea changamoto ya wananchi hao wanaodai wamefungwa wakiwa na watoto wadogo.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Luduga Hassan Ngella amesema kuwa hana taarifa ya wananchi hao kufungwa wakiwa na watoto wadogo na wenye matatizo ya kiafya na kuwataka kuendelea kutoa mchango wa ujenzi wa shule ya sekondari ya luduga.

Share:

Mawakili wa Zuma wajiondoa katika uwakilishi wake kabla ya kesi ya ufisadi kuanza

 


Bwana Zuma anakana mashiotaka yote dhidi yakeImage caption: Bwana Zuma anakana mashiotaka yote dhidi yake

Mawakili wa rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma wamewasilisha waraka wa kujiondoa katika uwakilishi wake.

Mawakili hao hawakutoa sababu ya kufanya hivyo.

Waraka huo uliwasilishwa Jumatano kufuatia hukumu ya wiki iliyopita ambapo rais huyo wa zamani alishindwa katika kesi ya rufaa dhidi ya azma ya taifa ya kutaka kupata pesa ambazo lilimgarimia kisheria Bw Zuma.

Hii inakuja kabla ya kuanza kwa kesi ya ufisadi inayotarajiwa kuanza tarehe 17 Mei.

Bw Zuma anakabiliwa na mashitaka 16 juu ya dola bilioni $2 (£1.4bn) za mkataba wa taifa wa silaha, ikiwa ni pamoja na wizi, utakatishaji wa pesa - mashitaka ambayo anayakana.

Share:

Chuo cha DON BOSCO Dodoma chaanza kutoa kozi ya kilimo cha kisasa cha Umwagiliaji


Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Chuo cha Ufundi Stadi cha DON BOSCO kilichopo jijini Dodoma kwa kushirikiana na ubalozi wa Israel hapa nchini na wadau mbalimbali kimeanza kutoa kozi ya kilimo cha kisasa kitakachoweza kuzalisha wataalamu wa kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kozi hiyo mpya katika chuo hicho Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ameitaka jamii kuchangamkia fulsa hiyo kwani ni fulsa mpya kabisa hapa nchini kupata kozi ya kilimo cha kisasa katika elimu kazi ya kati.

“Tukio hili ni muhimu sana hasa katika Mkoa wa Dodoma, mwanzo tulizoea kuona kozi za kilimo zilikuwa zikitolewa ngazi ya chuo kikuu ni niwachache waliokuwa na uwezo wa kufikia huko, lakini sasa DONBOSCO wameanza kutoa kozi hii ni fulsa kubwa wananchi waichangamkie hasa katika kilimo cha mboga mboga” amesema Dkt Mahenge.

Amesema kitendo cha nchi ya Israel kuleta wataalamu wa kufundisha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia teknolojia ni fulsa kwani hapo mwanzo tulikuwa tukipeleka wataalamu nchini Israel kwenda kusoma pia waliokuwa wakipata nafasi ya kwenda kusoma walikuwa wachache lakini sasa wataalamu wamekuja hapa nchini ni fulsa kubwa.

“Israel wao wamepiga hatua kubwa sana katika kilimo hasa cha umwagiliaji na mifugo kwahiyo wataalamu kuwapata hapa nchini ni fulsa kubwa sana, mwanzo waliokuwa wanapata nafasi walikuwa wachache kama nchi tulikuwa tunaweza kupeleka watu wa tano, lakini sasa kupitia DONBOSCO watapata fulsa hiyo wengi zaidi” amesema.

Amewataka wataalamu watakaopata elimu ya kilimo katika chuo hicho kwenda kuwa walimu kwa wengine huko vijijini katika jamii inayowazunguka hasa kupata elimu ya umwagiliaji kwa kutumia matone ambayo inapunguza upotevu wa maji hasa katika maeneo yenye upungufu wa maji ambapo wanaweza kuvuna maji ya mvua na kuyatumia katika kilimo hicho.

Ameongeza kuwa “tumepita katika lile shamba darasa naona hamjiamini kabisa katika katika kutoa mlivyofundishwa, ukifundishwa kit una ukakifahamu jitahidi kujiamini katika kuelezea unachokifahamu, hawa walimu wanaowafundisha wao wamepiga hatua kubwa katika kilimo kwahiyo wanajua” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha DON BOSCO Padri. Boniface Mchami, amesema chuo hicho kipo katika usajili wa VETA na kimekuwa kikitoa kozi mbalimbali ikiwamo ufundi bomba, uselemala, ufundi magari, kuchomelea vipuli, kushona, upishi na nyingine nyingi.

Amesema kwa sasa kwa kushirikiana ubalozi wa Israel, kupitia mradi wa CultAid na shirika la Innovation for Afrika na water for Mercy wameanzisha kozi mpya ya kufundisha kilimo cha kisasa kinachotumia maji machache na mfumo unaosoma kiwango cha maji yanayozalishwa na maji yanayotumika katika umwagiliaji shambani.

Amesema kozi hiyo itakuwa ya miezi nane 8 ambapo miezi 6 wataitumia kusoma darasani na miezi miwili wataitumia kufanya mazoezi kwa vitendo katika maeneo tofauti, huku akibainisha kuwa chuo kina shamba darasa lenye ukubwa wa ekari 6 yenye miondombinu yote ya kufundishia kama kisima, mfumo wa umeme na bwawa la kutunzia maji kabla ya kusukumwa kwenda shabani.

Nae Meneja mradi wa Innovetion Afrika Bi. Lerian Mosha amesema walianza shughuli zao hapa nchini mwaka 2006 katika utekelezaji wa miradi ya huduma za kijamii maeneo ya vijijini ambako mara nyingi hawapati fulsa kama hizo katika maji safi na umeme wa jua ambapo walianza katika Mkoa wa Pwani na sasa Dodoma.

Amesema kupitia mradi huo wamejiunga na chuo cha DON BOSCO ili kupitia utekelezaji wao waweze kusaidia teknolojia yao ya mfumo wa maji na umeme wa jua katika kutoa maji kisimani na kuyasukuma kwenda shambani kupitia mifumo hiyo.

Share:

Popular Posts

Copyright © MUUNGWANA BLOG | Powered by Blogger