Katika maisha ni vyema kama
utajua ni nini unataka na ukasimamia hicho. Hakuna mtu atakayekuambia kuwa hiki
ndicho unahitaji maishani mwako. Ni wajibu wako wewe mwenyewe kuhakikisha
unatambua hicho kitu na kuhakikisha unakiishi hicho. Maana katika dunia tulimo
kuna mambo mengi sana
yanayotokea kila mara ambapo usipokuwa makini ni rahisi kujikuta unapoteza
mwelekeo kabisa.
Mtu aliye kama bendera ni mtu ambaye yeye hajielewi, naweza
sema hajitambui kabisa, hajui kwa nini yupo hapa duniani, ni kama yupo tu kusindikiza
wengine, ndio maana anakuwa tayari kupelekeshwa kama
bendera, upepo unampeleka popote tu. Jua kile unataka ili ikusaidie
kutokuyumbishwa sana kama bendera, maana ukishajua nini unataka haijalishi
utakutana na nini, haijalishi kama upepo utakuwa mkali kiasi gani bado
hautakuondoa hapo, utabaki kwenye hilo kusudi lako la wewe kuwepo, labda
uniambie kuwa wewe uliumbwa bila kusudi maalumu, au wewe upo ili kuweza
kuufuata upepo kila unapoenda, lakini kila mtu anacho kitu anachotakiwa
kukifanya hapa duniani, kitafute hicho ili ufurahie maisha, usiishi bora upo
tu.
Kwa mfano tukiangalia hapa nchini hasa kipindi hiki cha
uchaguzi yapo mengi yanaendelea. Lakini usipokuwa makini na nidhamu ya kufanya
mambo unaweza kujikuta unafanya vitu au mambo ambayo hukupaswa kufanya kabisa,
kuna watu wanajihusisha na mambo ambayo hata hayawahusu kabisa. Wengine
wanaenda kwenye maeneo ya kazi kama picha tu maana muda wote wanautumia
kujadili hali inavyoendelea hapa nchini, waajiri wengi wanaibiwa sana muda wao kipindi
hiki. Wengine hata kwenye biashara zao wanashindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa
sababu ya yanayoendelea nchini, ni haki yako kufanya hayo lakini tumia na akili
ili kuhakikisha hiyo haki inakufaidisha zaidi pia na si kupoteza tu, ndio
namaanisha kupoteza huo muda unaotumia bila kuzalisha au kuingiza faida kwenye
shughuli unayopaswa kufanya, unageuka mwizi /fisadi bila kujijua maana unalipwa
ujira bila kufanya kazi inavyostahili.
Ni vyema utambue kuwa kuna maisha baada ya haya yote
yanayoendelea. Tambua kuwa utatakiwa uendelee kuishi na kuhusiana na watu ambao
labda mnatofautiana hata mitazamo katika kipindi hiki, hivyo usikubali
kupeperushwa tu kama bendera bali amua kuwa na msimamo , huwezi kuwa na msimamo
kama haujajua wewe ni nani, kwa nini upo, haujatambua thamani yako, ujue ulivyo
wa thamani, kwamba hakuna mwingine kama wewe, mwenyewe uwezo wa kufikiri na
kufanya mambo kama wewe, wewe ni wa pekee kabisa. Ndugu yangu ukishajielewa
hakutakuwa na upepo wa kukupeperusha maana utajua wapi usimame, wapi uwe kwa
wakati gani. Hii itakusaidia namna ya kuhusiana na watu, itakuwezesha hata
namna ya kukabili changamoto, ni rahisi hata kuishi na wengine kwa amani kama
wewe mwenyewe unajielewa, maana unakuwa haufanyi lolote kwa mashindano au
kutaka mtu fulani akuone au kukutambua kuwa u nani, haupo kwenye mashindano,
bali inakuwa ni wewe unaishi kama ulivyokusudiwa na muumba wako.
Hata kama utatofautiana mawazo/mitazamo na wengine
kujitambua kutakuwezesha kuheshimu kutofautiana kwenu, itakuwezesha kukubali
kutofautiana mtazamo juu ya jambo fulani, au mtazamo juu ya itikadi za kisiasa,
ikibidi kujadiliana kubali majadiliano na yawe ya hoja na si vinginevyo, usibishane
bali jadiliana. Kubishana hakuleti suluhu wala amani, lakini mkijadiliana
itafikia mahali mnaweza kukubali kutofautiana kwenu na kila mtu akabaki
anamheshimu mwenzie, kumbuka kuwa kuna maisha baada ya kila kitu, hivyo kitu
kimoja kisikufanye ukafunga milango ya kila kitu, pia kwenye kutofautiana ndio
kwenye kukua zaidi, maana ni wakati ambao tunapata fursa ya kufahamiana zaidi,
kujifunza zaidi n.k. Kuna maeneo ukimgusa mtu anajikuta kafunguka kila kitu na
unamwelewa zaidi , inakupa urahisi au uelewa wa jinsi ya kuzidi kuhusiana naye
wakati mwingine.
