Kwa sababu zao binafsi, kuna watu ambao wangependa kuajiriwa
maisha yao
yote. Au wangependa kuajiriwa kwa kipindi fulani kwenye maisha yao . Au kama ni mhitimu basi ungependa
kuajiriwa kama sehemu ya kuanzia kujijenga ili
baadae uweze kuingia kwenye kujiajiri au kufanya biashara ukiwa na uzoefu zaidi
ya sasa.
Hakuna mtu mwenye tatizo na hilo ,
iwe unataka kuajiriwa maisha yako yote au iwe unataka kuajiriwa kwa kipindi tu,
kama ndio kitu unachopenda kufanya, basi ni
vyema. Mafanikio hayaji kwa kufanya biashara au kuwa mjasiriamali tu, mafanikio
yanakuja kwa wewe kufanya kile ambacho unakifanya kwa ubora wa kipekee na kwa
utofauti sana .
Mafanikio yanakuja pale unapotoa thamani kubwa kwenye jambo lolote unalofanya.
Lakini pamoja na wewe kutaka kuendelea kupata kazi nzuri au
kutaka kuingia kwenye ulimwengu wa kazi, soko la ajira limechafuka vibaya sana . Nafasi za ajira ni
chache na wanaohitaji ajira hizo ni wengi mno. Kama
ni sifa kila mtu anazo, elimu kila mtu anasoma. Hivyo wasifu wenu wote
waombaji, yaani cv ni kama zinafanana. Ni
vigumu sana kusimama katikati ya kundi la wengi
na ukawa tofauti na kupata kazi bora kwa sababu tu cv yako umeiandika wewe ni
mchapa kazi, unajituma na maneno mengine kama
hayo ambayo kila mtu atayaandika.
Leo nataka nikushirikishe njia moja ambayo hakuna watu wengi
wanaoweza kuipita. Kwa wewe kupita njia hii utaongeza kitu kimoja kwenye cv
yako ambacho watu wengi hawana. Kitu hiki kitakusimamisha wewe na
kukutofautisha na kundi kubwa la watu wengine wanaotaka kazi unayotaka wewe.
Endelea kusoma na utajua kitu hiko muhimu sana .
Kama mmekwenda kuomba kazi, na sifa za mfanyakazi
anayehitajika ni kuwa na shahada ya kitu fulani, watakaoenda ni wengi sana . Kwa sababu watu
wengi sasa hivi wana shahada. Kwa wote kuwa na shahada wanaofanya usahili
watakuwa na wakati mgumu wa kuchagua ni nani apewe kazi, kwa sababu kama ni
kujieleza, kila mtu anaweza kuyapanga maneno yake vizuri sana na akajieleza
mpaka wanaofanya usahili wakasema huyu ndio mwenyewe. Lakini akiondoka na kuja
mwingine ambaye na yeye ameyapangilia maneno, wataona huyu naye yuko vizuri.
Mwisho wa siku, wanabaki na makaratasi ambayo karibu yote yanafanana na maneno
mazuri waliyoambiwa. Hivyo wanaweza kuchagua tu mtu yeyote. Na wewe ukakosa kwa
sababu tu ulikosa kitu cha kutofautisha.
Vipi kama ungekuwa na kitu cha kukutofautisha wewe na hawa
watu wengine. Vipi kama usingekuwa na haja ya kuongea sana bali kuonesha. Unapofika kwenye usahili
ukawaambia pia ninafanya kitu hiki na hiki kinachoendana na kazi hiyo ambayo
unaiomba? Na kuwa makini hapo nimekwambia unawaambia unafanya, sio ulifanya. Maana
hapa hatuleti zile hadithi kwamba nilikuwa kiranja, au nilikuwa mchezaji mzuri
shuleni, ni hadithi nzuri lakini kila mtu anaweza kuzisema pia. Wasahili
hawataenda kwenye kila shule kuuliza kama mtu
fulani alikuwa kiranja kweli.
Kwa hiyo nataka wewe uwe na kitu cha kuonesha, na unapoenda
kwenye usaili wa kazi unawaonesha, nimefanya na ninaendelea kufanya kitu hiki
kinachoendana na kazi hii ninayoomba kufanya. Ninachoweza kukuhakikishia kwamba
kama unachoonesha ni kitu kizuri, tayari kazi
utakuwa nayo, wengine watafanyiwa usaili ili kukamilisha tu zoezi ila wewe
utakuwa tayari na kazi. Unajua ni kwa nini? Kwa sababu ni wewe pekee
utakayekuwa na kitu cha kuonesha. Wengine watakuwa wavivu sana kuweza kuandaa kitu cha kuonesha, na
hata wewe binafsi huenda hutafanyia kazi kitu nitakachokuambia uende nacho
kuonesha.
Sasa ninaweza
kuonesha nini?
Taaluma niliyosomea sina cha kuonesha, labda mpaka nifanye
kazi ndio nitakuwa na kitu cha kuonesha. Kama
huu ndio utetezi wako basi huna utetezi. Kama kuna taaluma yoyote uliyosomea,
au kama kuna kitu ambacho unapenda kufanya
unaweza kuongeza hatua moja ya ziada tu na ukawa na kitu kikubwa cha kuonesha.
Kitu hiki wala hakihitaji uwekeze fedha za ziada, kitu ambacho utaniambia huna,
bali kinahitaji juhudi na maarifa yako ya ziada.
Kitu hiko ni nini? Kitu ninachotaka kukuambia hapa ni kwamba
uanzishe blog. Nianzishe blog? Ndio anzisha blog, hii itakutofautisha wewe na
watu wengine wengi watakaokwenda kuomba kazi na wewe. Blog ninayokuamia
uanzishe sio ya kuandika habari za udaku za dimond na wema, bali blog
itakayokuonesha wewe kama mtaalamu kwenye eneo
lile ambalo umesomea au unalopenda kufanyia kazi. Labda nitoe mifano michache
ambayo itakupa mwanga.
Umesomea uafisa wa jamii? Aisee wewe ndio unahitajika sana kwenye nchi hii.
Tuna matatizo mengi sana
ya kijamii, kuna unyanyasaji wa kijinsia unaoendelea, kuna malezi mabovu ya
watoto yanayopelekea taifa kukosa maadili na mengine mengi. Anzisha blog yako
na toa elimu hii ya kijamii.
Umesomea sheria? Hongera sana ,
kama utafungua blog utakuwa mkombozi wa wengi, mimi binafsi kuna sheria nyingi sana ningependa nizijue,
kila siku natafuta blog nzuri ya sheria sipati, ukianzisha nitakuwa msomaji
wako mzuri na pengine mteja wako pia. Ukweli ni kwamba wananchi wengi
wanahitaji msaada wa kisheria.
Chochote ulichosomea kuna maeneo mengi unayoweza kuandikia.
Kama hujaona ni wapi unapoweza kuandikia niandikie email kwenye
makirita@kisimachamaarifa.co.tz na niambie umesemea nini au unapenda kufanya
nini na nitakupa maarifa ya vitu vingi sana
unavyoweza kuandikia.
Kuna vitu vingi mno unavyoweza kuandika na kutoa elimu kwa
wengine. Unaweza hata kuandika mambo yanayofanyika hovyo kwenye eneo fulani
ambalo unalijua vizuri, au mambo yanayofanyika vizuri au njia mbadala za
kufanya kitu.
Na utakapokwenda kwenye usaili mwingine utawaambia pia mimi
ni mwanzilishi wa www.mimihapa.blogspot.com au www.mimihapa.com ambayo ni blog
inayotoa elimu kwenye eneo fulani la taaluma yako. Siku hizi kila mtu ana simu
janja (smartphone) wataichungulia na wakiona vitu vizuri pale, tayari kazi
unayo.
Ufanye nini sasa.
Fungua blog, nenda www.blogger.com na fungua blog yako. Huna
haja ya kuiremba sana , huna haja ya kuifanya
kubwa sana .
Kikubwa anza kuandika vitu vizuri ambavyo vitawasaidia watu. Na kadiri siku
zinavyokwenda utaendelea kuboresha. Kikubwa ifanye blog yako iwe ya kitaalamu
zaidi, yaani profesional, usiandike kitu chochote ambacho hakiendani na dhumuni
la blog, hata kama unaona wengi wangependa
kukisoma, yaani acha usiandike kabisa. Habari kama Lowasa ahamia CHADEMA ni nzuri
kwenye masikio ya watu, lakini usiweke kwenye blog yako, wewe ni mtaalamu,
fanya mambo ya kitaalamu.
Sijui chochote kuhusu
blog au kuandika.
Kumbuka sio lazima ununue kitabu hiki, unaweza kufanya kila
kitu mwenyewe, kama ni mjanja wa kutumia
kompyuta. Ila kama utataka kufanya mambo yako
kitaalamu zaidi, basi jipatie kitabu hiko. Na kama
hakitakusaidia chochote, utaniandikia kwenye namba hizo nikurudishie fedha
uliyolipia kitabu. Nakupa kitu ambacho kitaleta mabadiliko kwenye maisha yako,
ndio naamini hivyo na wengi waliokipata kitabu hiki wameshakuwa na blog zao na
wanaziendesha vizuri.
Unasubiri nini?
Unapomaliza kusoma hapa usisubiri kesho, sasa hivi nenda
www.blogger.com bonyeza create blog, andika jina la blog, unaweza kutumia jina
lako au hata jina lolote, ila liashirie kitu cha kitaalamu au kile unachoandika
na baada ya hapo weka makala yako ya kwanza, ya kuwasalimu wasomaji, kuwaambia
blog hiyo inahusu nini. Na endelea kuandika kila siku, NDIO KILA SIKU.
Samahani, nilisahau swali moja muhimu ambalo huenda
unajiuliza au unajipa sababu, SINA MUDA wa kuendesha blog. Sawa sio sababu
hiyo. Fanya hivi unahitaji kama nusu saa mpaka
saa moja kwa siku kuendesha blog yako. Unaipata wapi sasa, punguza kuzurura
kwenye mitandao na acha kabisa kuangalia tv, lala mapema na amka saa kumi na moja
au hata saa kumi asubuhi na andika kisha upost. Hivyo tu, kila siku. Kama
ungependa kuwa unaandika asubuhi ila ni mvivu sana
tuwasiliane, ninaweza kukusaidia kwenye hilo
pia.
