Mshtuko! Bi harusi Agnes Omari (26) amezua kizaazaa baada ya
kudaiwa kupandisha mashetani kanisani wakati akivishwa pete ya ndoa, hali
iliyosababisha tendo la kufungishwa ndoa kusimama kwa muda kwa ajili ya
kutafuta msaada wa maombi.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, bwana harusi, Arnold Martin
alisema sakata hilo
lilijiri hivi karibuni kwenye Kanisa Katoliki la Parokia ya Mbagala-Zakhem
jijini Dar.
Alisema kwamba, alipata taarifa usiku wa kuamkia siku ya
ndoa kutoka kwa msimamizi wa bi harusi kuwa mchumba’ke amepandisha mashetani,
tatizo ambalo hakuwa nalo katika kipindi chote walichoishi pamoja.
Kutokana na tatizo hilo , Arnold alisema alivunja
utaratibu na kwenda kumuona mchumba’ke huyo na kumkuta akijigaragaza huku
akipiga makelele na kuzungumza lugha za ajabu.
“Kulipokucha, hali yake ilionekana kuwa nzuri kiasi kwamba
majira ya saa 3:00 asubuhi, aliondoka na msimamizi wake kwa ajili ya
kubadilisha gauni la harusi maeneo ya Mbagala-Kizuiani baada ya lile la awali
kuonekana kumbana huku na mimi nikijiandaa kwenda saluni,” alisema Arnold .
Baada ya kutoka na msimamizi wake huyo, haukupita muda mrefu
akapigiwa simu kuwa hali hiyo imejirudia, akamfuata na kumbeba kwenye gari lake kisha
kumkimbiza katika Parokia ya Mbagala-Zakhem kwa ajili ya msaada wa maombi na
kutoa taarifa kwa paroko kuhusu hali ya mchumba’ke huyo.
Bi harusi huyo aliombewa lakini wakati akimvisha pete ya
ndoa kanisani hapo hali hiyo ilijirudia ndipo alipohamishiwa katika Kanisa la
Nabii Yaspi lililopo Buza-Kipera jijini Dar ambapo wakiwa huko, walikutana na
wachungaji ambao waliwaombea na hali ikatulia.
“Hali hiyo ilijirudia tena wakati tukipiga picha palepale
kanisani akaanza tena kupandisha mashetani, akaombewa lakini hali ilizidi kuwa
mbaya, wakaja watu wa Karismatiki nao ikashindikana ikabidi tufunge safari tena
kuelekea kulekule kwa Nabii Yaspi ambako aliombewa, akapona.
“Wakati tukiingia ukumbini, hali hiyo ilijirudia tena ambapo
sherehe nzima iliharibika na kuwa majonzi hivyo kila mtu akaondoka kimyakimya.
“Bi harusi aliondoka na ndugu zake usiku ule hadi kesho yake
nilipoambiwa amerudia hali yake ya kawaida ila kinachonishangaza nilipoenda
pale nyumbani kwao alikuwa akionesha kama vile hanifahamu kabisa pamoja na
kwamba nilifunga naye ndoa,” alisema Arnold
ambaye alidai kuwa anatarajia kurudi tena kwa Nabii Yaspi ili kumaliza tatizo hilo .
