Habari za siku rafiki
na mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Nimatumaini yangu
umzima wa afya na unaendelea kujifunza ili kuboresha maisha yako. Karibu tena
katika siku nyingine ambapo tunapata fursa ya kujadili mambo ya kimafanikio kama ilivyo kawaida yetu.
Katika makala yetu ya leo tutaangalia kuhusu afya kama
sehemu muhimu sana
kwa mafanikio yoyote yale. Bila shaka utakubaliana nami kuwa kama
afya yako ni mbovu huwezi kufanikiwa hata iweje. Mafanikio yote unayoyatafuta
yanahitaji uwe na afya njema ili kuyafikia, vinginevyo utakwama.
Ikumbukwe kuwa hakuna mtu anayependa kuumwa au afya yake
kuwa mbovu hata kidogo. Kila mtu anahitaji afya yake iwe bora tena hata siku
zote ikiwezekana ili kuishi maisha ya furaha. Lakini ubora huo wa afya
tunaoutaka hauji hivihivi tu huwa zipo kanuni au siri za kufanya ili kuweza
kujijengea afya bora zaidi.
1. Fanya Mazoezi ya
mwili kila siku.
Mazoezi ya mwili ni ya muhimu sana kwa afya yetu na yanafaida nyingi kwetu.
Unapofanya mazoezi hiyo inakuwa inakusaidia kuupa mwili afya kutokana na ukweli
kwamba yanapunguza magonjwa mengi kama ya
msongo wa mawazo na shinikizo la damu. Hivyo unapofanya mazoezi hata kama ni kidogo unakuwa upo katika hali nzuri kiafya
tofauti na yule ambaye hafanyi kabisa.
2. Pata muda wa
kupumzika
Baada ya kazi zetu tunazozifanya, mwili huu ni lazima
upumzike ili upate kujitengeneza upya wenyewe. Yatupasa kuwa na muda wa
burudani na wa kupumzika ili kupunguza msongo utokanao na kazi pamoja na
majukumu ya kifamilia. Bila kuwa na muda wa kutosha kupumzika mara nyingi watu
wanakuwa na wasiwasi, mfadhaiko na hasira kali.
Hivyo ni lazima kutenga muda huu ili kujijengea afya bora.
3. Kula chakula bora.
4. Epuka Vitu
Vinavyokuletea Madhara.
Vitu hivi inaweza ikawa ni pamoja na matumizi mbaya ya pombe
hususani pombe kali au uvutaji wa sigara wa kupitiliza. Unapokuwa unafanya
mambo kama hayo tambua tu moja kwa moja
yatakuharibia afya yako. Kitu cha msingi hapo ni kuhakikisha unaachana na tabia
hiyo ili kujijengea afya bora na endelevu kwako.
5. Kunywa maji safi na ya kutosha.
Tunapozungumzia afya safi
huwezi kulikwepa hili la kunywa maji safi .
Unalazimika kunywa maji safi
na ya kutosha ili kuipa akili yako nguvu ya kufanya kazi kwa ufanisi. Unapokunywa
maji mengi yanakuwa yanasaidia ubongo wako kufanya kazi vizuri kwa sababu
yanakuwa yanaiongezea akili yako oksijeni kwa hali ya juu kabisa.
6. Dumisha usafi.
Usafi ni suala la muhimu sana katika kuboresha afya zetu. Usafi huu
unaweza ukaanzia kwenye miili yetu, mavazi na hata pia katika mazingira yetu.
Tunapoimarisha usafi katika maeneo yote hayo inakuwa ni rahisi kuweza
kukabiliana na magonjwa mbalimbali ambayo yangeweza kutushambulia.
Kumbuka, kuwa na afya
bora ni msingi mkubwa wa mafanikio kwa binadamu. Hivyo ni lazima kwetu
kudumisha afya bora siku zetu ili kujihakikishia hata usalama wa maisha yetu
kwa kiasi kikubwa.
