Mwenyekiti wa Chadema, mh Freeman Mbowe amemtaka Rais Kikwete kutovuruga amani ya
nchi na badala yake amemtaka
aondoke madarakani na kuiacha
nchi ikiwa salama.
Mbowe alitoa kauli
hiyo jana jioni katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mbogwe, wilayani
Geita.
Alisema Rais Kikwete
anatakiwa aondoke madarakani salama kama
walivyofanya marais wenzake wastaafu.
“Rais Kikwete ameamua kuwa mpiga debe wa Magufuli (mgombea
wa CCM), sasa mimi naomba nimjibu yeye kama
mpiga debe na si rais,” alisema Mbowe.
Alisema Rais Kikwete ameamua kuwaaminisha Watanzania kuwa wapiga kura wapo milioni 28
badala ya milioni 22 kama ilivyotangazwa na
Tume ya Taifa ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
“Sasa nataka kumuuliza Rais Kikwete hao wapiga kura wengine
milioni sita wametoka wapi?” alihoji Mbowe na kuongeza:
“Naomba kumwambia Rais Kikwete kuwa hii nchi si yake, hii
nchi si ya CCM na hii nchi si ya familia yake...hii ni nchi ya Watanzania,”
alisema.
Alisema hatua ya Rais Kikwete na CCM inayoungwa mkono na Nec
kuwataka wananchi wapige kura na kuondoka vituoni haiwatendei haki Watanzania.
“Kikatiba Watanzania wana haki ya kulinda kura zao kwa
sababu zile ni kura zao, nashangaa Rais Kikwete anawaambia watu waondoke,”
alisema.
Mbowe, aliwaomba Watanzania wote kwenda kwenye vituo kwa
ajili ya kupiga kura ikiwa ni pamoja na kuzilinda kura zao.
Pia alisema anashangazwa na kauli ya Rais Kikwete ya
kuliagiza Jeshi la Polisi kuwaondoa wananchi kwa nguvu katika vituo vya kupigia
kura.
“Hao askari walioagizwa na Rais Kikwete, nao wana watoto na
familia zao, naomba nikwambie Rais Kikwete kuwa huwezi kuzuia mabadiliko.
Zimebaki siku 11, Mungu atajibu maombi yetu...nawaambia wananchi nendeni
mkapige kura kaeni mita 200 lindeni kura zetu,” alisema.
Akiwa mjini Dodoma
jana wakati wa kilele cha Mwenge wa
Uhuru kilichoenda sanjari na kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais
Kikwete alitaja idadi
kubwa ya wapiga
kura kuliko iliyotolewa
na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi.
Hata hivyo, jana jioni
Ikulu ililitolea ufafanuzi
suala hilo na
kudai kuwa idadi
kamili ya wapiga
kura ni milioni 22
na si vinginevyo.
"..... Katika Kilele cha mbio za mwenge wa uhuru ,
kumbukumbu ya Baba wa Taifa , Mwalimu JULIUS Nyerere na wiki ya vijana Kitaifa,
Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba
yake amezungumzia idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura.
"Kwa uhakika amesema kuwa idadi ya wapiga kura ni
22,751, 292 kwa upande wa Bara na 503,193 wa Zanzibar .
Hii ndiyo idadi kamili ambayo imo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais na
hii ndiyo idadi kamili kama ilivyotolewa na Tume ya Uchaguzi Tanzania .." Ilisema
Sehemu ya Tamko
hilo la Ikulu
jana.
