Mikoa tisa ndiyo itakayoamua mshindi wa kinyang’anyiro cha
urais, Mwananchi inaweza kukuthibitishia.
Mgombea aliyechanga karata zake vyema kwenye mikoa hiyo,
atakuwa na uwezo wa kuvuna takriban kura milioni 12 ambazo haziwezi kupatikana
kwenye mikoa mingine 21 iliyosalia, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Mapema wiki hii, NEC ilitangaza idadi ya mwisho ya
wapigakura waliojiandikisha kuwa ni milioni 22.75 watakaogawanywa katika vituo
65,105, kila kimoja kikiwa kimepangiwa wapigakura wasiozidi 450.
Kutokana na mgawanyo wa wagipakura hao kwa mikoa yote 30
nchini, Mwananchi limekokotoa na kubaini kuwa mikoa tisa yenye idadi kubwa ya
wapigakura inaweza ikaamua mshindi kutokana na kila mmoja kuwa na zaidi ya
wapigakura milioni moja.
Mikoa hiyo ni Dar es Salaam ,
Mbeya, Mwanza, Morogoro, Tabora, Dodoma ,
Kagera, Tanga na Arusha.
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli na wa Chadema, Edward
Lowassa wamekuwa wakizungukia mikoa mitatu kati ya hiyo - Dar es Salaam , Arusha na Mbeya - kwa nyakati
tofauti, wakiingia na kutoka isipokuwa Mwanza pekee ambako wote wawili walisita
kuingia wakisubiri ngwe ya mwisho.
Mkoa unaoongoza kwa idadi kubwa ya wananchi waliojiandikisha
kupiga kura ni Dar es Salaam
wenye wapigakura 2,775,295 ukifuatiwa na Mwanza (1,448,884), Mbeya (1,397,653)
na Morogoro (1,271,951).
Idadi ya wapiga kura kwenye mikoa mingine ni Tabora
(1,097,760), Dodoma
(1,071,383), Kagera (1,051,681), Tanga (1,009,753) na Arusha (1,009,292). Mikoa
hii pekee inatoa ushindi wa zaidi ya asilimia 53 ambao unatosha kumpeleka
mgombea husika Ikulu.
Dar es Salaam yenye zaidi ya asilimia 10 ya wapigakura wote
imevutia macho ya vyama vyote vikubwa ambavyo licha ya kuzindulia kampeni zake,
pengine vitalazimika kufungia kampeni zao za uchaguzi pia.
Umuhimu wa Dar es
Salaam ni kwamba yeyote atakayepata kura nyingi, hata
akikosa katika mikoa minane iliyobaki, anaweza akashinda akifanya vizuri kwenye
mikoa 21 iliyobaki ambayo ina takribani wapigakura milioni 10.
Ukiacha mikoa yote ya Zanzibar ,
mikoa minane yenye idadi ndogo zaidi ya wapigakura ambayo ni sawa na asilimia
18.6 tu kwenye ushindi wa rais, ni pamoja na Katavi (322,127), Njombe
(383,366), Rukwa (459,573), Lindi (514,558), Iringa (529,887), Singida
(648,897), Manyara (678,586) na Pwani (697,533).
Mikoa mingine yenye kura nyingi ambazo pia zinachangia kwa
kiwango kikubwa kwenye ushindi kwa asilimia 28.4 ni Mara (892,741), Geita
(887,982), Kilimanjaro (800,349), Kigoma (792,551), Shinyanga (773,273), Ruvuma
(739,774), Mtwara (728,981) na Simiyu (718,777).
Wapigakura wote 503,193 wa Zanzibar watalazimika kupiga kura mara tano
ikiwa ni kura za rais wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ), mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi, sheha, mbunge na rais wa Muungano. Kati ya hao 48,182 watafanya
hivyo kwa rais wa Muungano na mbunge pekee.
Mkurugenzi wa Daftari la Kudumu la Wapigakura na Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa NEC, Dk Modestus Kipilimba alisema uhalali
wa wapigakura wa Zanzibar
unatokana na taratibu zilizopo visiwani humo.
“Kuna sheria ya
uchaguzi inayomtambua anayeruhusiwa kuchagua mbunge na Rais wa Muungano huku
ikimzuia kufanya hivyo kwa viongozi wa visiwani pekee. Yule anayechagua
viongozi wa Zanzibar anaruhusiwa kwa wote, hivyo hao 48,000 wamebanwa na vigezo
vilivyowekwa,” alisema.
