Didii, Uaminifu, Ukweli na imani, Nguzo Kuu za MAFANIKIO

NAMSHUKURU Mungu wa Mbinguni kwa kunijalia afya njema na uwezo wa kufanya kazi, namshukuru kwa neema na baraka zake katika maisha yangu ya kila siku, namshukuru kwa muongozo anaonipa katika kuishi na watu wanaonizunguka.

 Nampenda kama anavyonipenda na ninamshukuru kwa kunipa nafasi nyingine kila siku niweze kufikiria toba ya kweli ili nitakapolala nipumzike katika amani ya milele nikiwa upande wa mkono wake wa kuume.

Kwa mnaokumbuka wiki iliyopita tuliongelea juu ya jinsi ya kuishi vizuri na wafanyakazi wenzako huko maofisini, naamini ni mada iliyowagusa wengi kwani wingi wa simu nilizopokea siku hiyo zinathibitisha hilo, nasema niko katika kona hii kuleta tiba ya mafanikio bora maishani na kupandikiza mbegu ya ushindi kwa kila Mtanzania aliyekata tamaa na maisha.

Katika maisha, hakuna kitu kinachoweza kufanyika kama hakutakuwa na bidii ya utendaji.

Huo ndiyo ukweli, bidii ni kiungo muhimu sana katika kufanikisha jambo lolote kwa mtazamo chanya.

Lakini bidii peke yake inatosha kukamilisha mafanikio maishani? Jibu ni kwamba si kweli kwani pamoja na bidii kuwa kiungo muhimu cha mafanikio, lakini bado kuna vitu vingine muhimu zaidi ili kujipatia maendeleo na mafanikio maishani ambavyo ni Uaminifu, Ukweli na Imani.

Vitu hivi kwa pamoja vinakamilisha nguzo kuu muhimu maishani kwa mtu aliyedhamiria kupata mabadiliko. Katika kila jambo unalofanya, hakikisha kuwa unalifanya kwa bidii huku akili na nguvu zako zikiwa kwa asilimia 95, ukifanya hivyo lazima utapata mafanikio.

Baada ya kuwa na bidii kwa kiwango hicho, jambo linalofuata ni uaminifu wako katika mazingira unayofanyia kazi. Kumbuka kuwa uaminifu haujali kama wewe ni mfanyakazi au mfanyabiashara bali kwa kila eneo unalofanyia kazi hakikisha kuwa unakuwa muaminifu kwa kiwango kikubwa. Uaminifu katika kazi zako lakini pia uaminifu kwenye mali za wengine.

Mathalani bosi wako amekuagiza kufanya jambo linalohitaji fedha nyingi, basi usifanye ujanja wowote kuzidisha kiwango cha kawaida kwani kufanya hivyo si ujanja badala yake ni kujiwekea mazingira magumu sana maishani.

Hivyo uanimifu ni nguzo nyingine muhimu sana katika safari ya kutafuta mafanikio maishani mwako.

Unapokopa fedha au kitu flani kwa mtu, hakikisha unakirejesha kwa muda mliokubaliana, achana na tabia ya kudhulumu vitu ambavyo si halali kwako kwani utafiti wa kisaikolojia unaonesha kuwa, mali zote zinazopatikana kwa njia za mkato au njia ambazo si za uaminifu mara nyingi huwa hazidumu.

Hivyo msomaji wangu, jitahidi sana kuboresha eneo la uaminifu katika mazingira unayojipatia riziki maishani mwako.

Lakini pia, nguzo nyingine ni Ukweli kwani ukitaka kuishi maisha ya amani na yenye furaha basi jitahidi sana kusema ukweli kwa kila sentensi inayotoka kinywani mwako. Katika ofisi ninayofanyia kazi, ninashika nafasi ndogo sana ya uongozi lakini kitu ambacho huwa nasisitiza kwa wafanyakazi wenzangu ni kusema ukweli.

Achana na ahadi ambazo unajua kabisa kwamba huwezi kuzitimiza kwani ukijijengea mazingiara ya uongo katika jamii unayoishi basi utakuwa unafukuza myanya ya mafanikio maana unaweza kuwa na kitu cha muhimu sana kukifanya lakini kwa kuwa umejijengea  mazingira ya uongo basi hakuna atakaye kuamini.

Ukiwa msemakweli, hautalaumiwa na mtu na wala hutamlaumu mtu.
Mfano, rafiki yako anakuomba umfanyie jambo flani kwa wakati maalum na wewe unakubali japo unakuwa na uwezo mdogo kufanya hivyo, unafikiri kama muda  ukifika na haujafanya kitu hicho ni nini kitafuata? Jibu ni lawama kwani umeahidi kitu ambacho huwezi kukifanya na siku nyingine hawezi kukuamini.

Juu ya hayo yote kuna kitu muhimu zaidi ambacho ni Imani.
Hapa ndipo kwenye kiini kikubwa cha mafanikio maishani kwani hata kama unafanya kazi kwa bidii kiasi gani, ni mkweli kwa kiasi gani lakini kama hauna imani na unachokitaka basi ni vigumu kufanikiwa.

Yaani kama wewe unataka kuwa mwanasheria lakini huna imani na ndoto yako, basi elewa ni vigumu mno kufanikiwa katika hilo.