F Kimakonde cha Cheka gumzo India | Muungwana BLOG

Kimakonde cha Cheka gumzo India


Dar es Salaam. Bondia namba moja nchini, Francis Cheka amewateka mashabiki wa ngumi India kutokana na kuzungumza nao kwa Kimakonde.

Tukio hilo lilitokea jana wakati bondia yuko na mpinzani wake Vijenger Singh walipoitwa mbele ya vyombo vya habari na kuonyeshwa mkanda wa ubingwa wa WBF wa mabara atakaogombea keshokutwa.

Cheka aliliambia gazeti hili kwamba alitumia mbinu hiyo ya kuzungumza kimakonde ili kumshtua mpinzani wake huku akicheka na kueleza kuwa mbinu hiyo ilimchanganya mpinzani wake pamoja na mashabiki.

“Napenda kuzungumza Kimakonde ni lugha yangu ya asili,” alisema Cheka akieleza kwamba alichokizungumza ni kwamba bondia huyo aliyewahi kuwa bingwa wa Olimpiki hafiki mbali Jumamosi.

“Niko fiti, sitawaangusha Watanzania, kuna baadhi ya watu wanadhani kiwango changu kimeshuka ni kweli kilishuka wakati nikiwa jela, lakini sasa siyo yule Cheka wa mwaka jana. Mashabiki wangu wajiandae kunipokea na mkanda baada ya pambano hili,” alitamba Cheka kwa kujiamini.

Cheka amefuatana na meneja wake, Juma Ndambile, kocha Abdallah Salehe ‘Commando’ na msaidizi wake, Jay Msangi, ambaye pia ndiye mkalimani wake.

Cheka na Singh watazichapa Jumamosi katika pambano la raundi 12 la uzani wa super middle (kilo 76) la ubingwa wa mabara wa WBF.

Bondia huyo alitarajiwa kulipwa Euro 8,000 (Sh18.4 milioni) hata kama atapigwa, huku akitarajiwa kuwania taji kubwa zaidi endapo atashinda.

Cheka aliyekuwa amevalia suti ya kijivu, shati jeupe na tai alionekana kuwa fiti zaidi ya mpinzani wake mwenye rekodi ya kuiletea Uingereza medali ya dhahabu ya Olimpiki kabla ya kujiunga na ngumi za kulipwa.