Mkuu wa mkoa wa Geita awataka wafanyabiashara wa mazao katika mkoa wake kutouza nje ya mkoa.

Mkuu wa mkoa wa Geita Meja Jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga amewataka wafanyabiashara wa mazao katika mkoa wake kutouza bidhaa hizo nje ya mkoa ili kukabiliana na upungufu wa chakula uliosababishwa na kupungua kwa mvua za vuli.

Kyunga ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua maghala ya vyakula na kufanya tathimini ya hali juu ya upatikanaji wa chakula kutokana na tishio la njaa katika baadhi ya mikoa ya Tanzania, amesema kutokana na hali ya mabadiliko ya tabia nchi tayari kuna baadhi ya wafanyabiashara kutoka mikoa na nchi jirani wanafika mkoani Geita kununua mazao hivyo itasababisha mazao kupanda bei na hatimaye kuisha kabisa na baa la njaa litaukumba mkoa huu pia.

Akitoa ripoti ya mvua za vuli zilizoanza kunyesha mwezi Oktoba 2016 mkuu wa wilaya ya Bukombe Josephat Maganga amesema kutokana na kupungua kwa mvua tofauti na miaka mingine wilaya imeanza kutoa elimu kwa wananchi kuanza kulima mazao yanayoweza kuhimili ukame.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wafanyabiashara wamesema bidhaa za chakula zinapatikana japo kwa sasa zimeanza kupandishwa bei, aidha wamewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato badala ya kukaa vijiweni na kulalamikia hali ngumu ya uchumi.
Mpya zaidi Nzee zaidi