Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa
POLISI mkoani Dodoma wamebaini ujanja wa wafanyabiashara wa viroba wa kuficha bidhaa hiyo kwenye maghala yasiyotumika kwa kuogopa kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika kampeni hiyo endelevu iliyofanywa mjini Dodoma na Mpwapwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Machi 9, mwaka huu, ilikamata jumla ya katoni 2,199 za viroba zenye thamani ya Sh milioni 134.9.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa aliongoza kundi la polisi na waandishi wa habari kwenda kushuhudia shehena ya viroba katoni 1,690 yenye thamani ya Sh milioni 126.8 iliyokuwa imefichwa eneo la NaneNane umbali wa kilometa tano kutoka mjini.
HabariLeo imeshuhudia shehena ya viroba mali ya Consolatha Malya (58), ambayo ilikuwa imefichwa kwenye ghala moja mali ya Lelo Massawe katika eneo la Nane Nane ambalo lilikuwa halitumiki.
Consolatha ambaye ni mkazi wa Area C , mjini Dodoma pia ni mmiliki wa Kampuni ya Cowike Enterprise Limited, aliamua kuficha viroba hivyo kukwepa kushikwa.
Consolata alisema, alinunua shehena hiyo kabla ya serikali haijatangaza kupiga marufuku vinywaji hivyo vilivyo katika mifuko ya plastiki, akaahidi kutunza na kusuburi maagizo ya serikali kuhusu shehena hiyo.
Kamanda Mambosasa alisema polisi pia walikamata shehena ya viroba katoni 444 vyenye thamani ya Sh milioni 36 mali ya Siloya Mbonyi (39) ambaye ni mfanyabiashara na mmiliki wa Kampuni ya Takawedo Investiment Limited ya mjini Mpwapwa.
Kamanda alisema pia walikamata viroba katoni 62 na vilivyofunguliwa 25 vyenye thamani ya Sh milioni 4.5, mali ya Jobu Matonya (53), mkazi wa Mpwapwa Mjini.
Polisi mkoani Dodoma wamefanya msako wa kukamata viroba mara mbili katika wiki hii, katika tukio la kwanza, walikamata takribani katoni 2,000 za Festo Mselia ambaye aliamua kujiua mwanzoni mwa wiki na jana walikata jumla ya katoni 2,199 za wafanyabiashara watatu.
