Serikali Inampango wa Kutengeneza Mwongozo Wa Kuwarudisha Shule Waliopata Mimba

Mkurugenzi Msaidizi Masuala Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Venance Manori akiwa katika picha ya pamoja na waandaaji wa warsha ya kuwawezesha Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita za Afrika katika kutengeneza mipango inayozingatia usawa wa kijinsia katika elimu kutoka shirika la Plan International- Tanzania, Global Partnership for Education (GPE), Dubai Cares pamoja na United Nations Girls’ Education Initiative (UNGEI) mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Serikali imejipanga kutengeneza mwongozo wa kuwarudisha shuleni wanafunzi waliopata mimba wakiwa masomoni ili kuhakikisha wanapata elimu hadi kufikia ngazi za juu.

Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Masuala Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Venance Manori alipokuwa akifungua warsha ya kuwawezesha Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita za Afrika katika kutengeneza mipango inayozingatia jinsia katika elimu kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Prof. Joyce Ndalichako.

Manori amesema Serikali ya Tanzania inajitahidi kuzingatia jinsia katika utoaji wa elimu ambapo takwimu zinaonyesha kuwa elimu ya Msingi na Sekondari uwiano wake ni moja kwa moja japo kuwa idadi ya wasichana hupungua kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakumba hivyo lengo la warsha hiyo ni kuwasaidia wadau kuweka mipango ya elimu inayozingatia usawa wa kijinsia.

“Serikali yetu imejipanga kuhakikisha wasichana wanapata elimu hadi ngazi za juu lakini mpango huo unakumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za mimba na ndoa za utotoni hivyo ili kuhakikisha mtoto wa kike anafikia ngazi za juu za elimu tuko kwenye mchakato wa kuandaa mwongozo kwa ajili ya wanafunzi waliopata mimba wakiwa bado wanasoma kupata nafasi ya kuendelea na masomo,”alisema Manori.