Taarifa ya Siku ya Saba ziara ya mahsusi ya kimazingira ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe January Makamba kutembelea mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania yenye lengo la kung’amua changamoto za kimazingira, athari za mabadiliko ya tabia nchi ili kuweka mikakati sahihi ya kukabiliana na changamoto hizo kwa kushirikisha ngazi zote za serikali pamoja na wadau wote wa mazingira.
Ikiwa ni siku yake ya pili katika mkoa wa Kilimanjaro, Waziri Makamba ametembelea kiwanda cha saruji cha Moshi (Moshi Cement) kilichopo wilayani Rombo ambapo amekagua hali ya utunzaji, uhifadhi na uzingatiaji wa sheria za mazingira katika kiwanda hicho.
Katika ziara hiyo Waziri Makamba amebaini kuwa mashine za kuzuia vumbi linalotokana na shughuli za uzalishaji katika kiwanda hicho hazifanyi kazi ipasavyo hivyo vumbi linalotoka kuchangia kwa kiasi kikubwa kuchafua mazingira na kuhatarisha afya za wananchi jirani na maeneo ya kiwanda.
Kufuatia ukiukwaji huo wa taratibu na uchafuzi wa mazingira Waziri Makamba ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kukisimamisha kiwanda hicho mara moja kuendelea na uzalishaji hadi pale taratibu stahiki kama zinavyotakiwa na sheria za mazingira zitakapofuatwa.
Waziri Makamba pia ametembelea na kukagua eneo la Ziwa Challa katika Kijiji cha Malowa wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, ziwa ambalo liko mpakani mwa Kenya na Tanzania na ambalo utunzaji wake unategemea kwa kiasi kikubwa jitihada za nchi zote mbili.
Licha jitihada kubwa zinazofanywa kwa sasa katika kulitunza ziwa Challa Waziri Makamba ameeleza kuwa Serikali na Ofisi ya Makamu wa Rais zinafanya jitihada za kuhifadhi mazingira katika maziwa ya ndani (inland lakes) ikiwemo kuhakikisha shughuli zinazofanywa katika eneo la ziwa zinafanyiwa tathmini ya athari za mazingira ili kuhakikisha hazina athari kwenye ziwa.
“kuna utafiti unaofanyika sasa wa kugundua athari za mabadiliko ya tabia nchi, ukilenga kutambua ni kwa namna gani na kiasi gani kupungua kwa kina cha ziwa kunatokana na mabadiliko ya tabia nchi na mara utafiti utakapokamilika hatua stahiki za kuchukuliwa zitapendekezwa” Alifafanua Waziri Makamba.
Vilevile ameahidi kufanya kufanya mazungumzo na mamlaka husika katika serikali ya Kenya ili kuweka mikakati ya pamoja itakayolenga kulinda na kutunza mazingira ya eneo hilo na rasilimali nyingine ambazo zinapatikana katika nchi zote mbili.
Akimaliza ziara yake katika mkoa wa Kilimanjaro, mkoa ambao mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote Afrika unapatikana Waziri ameeleza kuwa dhamana ya Mlima Kilimanjaro ni kielelezo kikubwa cha hali ya mazingira sio tu nchini bali Afrika na Duniani kwa ujumla na kwamba theluji katika mlima huo inaeleza ni kwa kiasi gani jitihada za utunzaji wa mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi zinazofanywa zinafanikiwa au la. Amesisitiza kuwa upungufu wa theluji katika kilele cha mlima huo hivi sasa unaonyesha dhahiri ni kias gani bado kuna kazi kubwa katika kusimamia uhifadhi wa mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
