Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe ametoa wito kwa wasanii nchini kutovuka mipaka katika utengenezaji wa kazi zao mpaka kufikia hatua ya kuvunja Sheria na taratibu za nchi.
Ameyasema hayo Mjini Dodoma jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego kwa mwaliko wa Waziri huyo.
Amesema kuwa wasanii ni nguzo muhimu katika nchi sio kwa kufanya kazi ya kuburudisha na kuelimisha bali katika kuujenga Utamaduni wa nchi ambao ndio nguzo muhimu sana kwa malezi na makuzi ya wanajamii.
“Niwaombe wasanii nchini kuzingatia Sheria na taratibu za nchi katika utunzi wao na utenegenezaji wao wa kazi zao” Alisisitiza Mhe. Dkt Mwakyembe.
Aidha ameongeza kuwa Serikali haina nia ya kuwanyima uhuru wa kujieleza bali watambue kuwa nchi inaendeshwa kwa taratibu na Sheria ambazo zinatakiwa zifuatwe na watu wote.
