Mlinzi abuni roboti baada ya ujambazi kijijini kwao

"Wakati natafakari kwanini walimpiga mtoto risasi ya mguuni aliyeshika tochi, ndio matokeo yake haya leo," ndiyo kauli ya awali wa kijana, Brighton Katabazi (29), mhitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), katika fani ya Elektroniki na Mawasiliano.

Katabazi anasema kuwa amebuni roboti ya mfano wa mtu, ambayo ina uwezo wa kushika tochi mkono wa kushoto, baada ya kuongozwa na mitambo aliyobuni.

Katabazi ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kasanda katika wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma, alihitimu UDSM mwaka 2014 na kutunukiwa Shahada ya Kwanza ya Elektroniki na Mawasiliano.

Historia yake ni kwamba, aipata elimu ya sekondari katika shule ya Kasanda na kisha aliendelea na kidato cha tano na sita, Pugu sekondari jijini Dar es Salaam.

Anasema binasfi ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto saba, wote wavulana, yeye akiwa pekee aliyebahatika kupata elimu ya juu.

Katabazi anasema kuwa mama yake ni mkulima, huku akimsifu kuwa ni ‘mama bora’ baada ya kufanikisha kuilea familia yake na kujitegemea, licha ya mumewe kufariki miaka mingi iliyopita.

TUKIO LA UJAMBAZI

Katabazi anayeonyesha wajihi wa upole, lakini akiwa na weledi wa kujieleza, anasema kuwa mwaka 2015 baada ya kuwepo tukio la ujambazi kijijini kwao, alifikiria mbinu za kutafuta suluhisho kijijini na kwingineko.

Anaeleza kwamba majambazi hayo yalivamia kwenye nyumba ambayo haipo mbali na mahali anapoishi yeye kijijini.

“Majambazi yaliingia kwenye nyumba majira ya saa mbili usiku, wakaiba pesa na kutoweka. Wakati wanakimbia, kwa kuwa kijijini ni giza maeneo mengi, nyumba nyingine kulikuwa na mtoto yuko nje anachezea tochi, akamulika.

“Majambazi hao walipoona huo mwanga walimfyatulia risasi na kumkuta mguuni,” anasimulia tukio hilo la kuhuzunisha.

Katabazi anasema baada ya hapo mtoto yule alikimbizwa hospitali, naye akirejea nyumbani akitafakari sana tukio hilo la kikatili dhidi ya mtoto na namna ya kulidhibiti, kupitia na nafasi yake binafsi ya uhandisi.

AUNDA ROBOTI

Anasema ubunifu huo aliutekekeza kwa matumizi ya vifaa vya kawaida, ili kuunda kitu chenye mwonekano mithili ya mtu.

Katabazi anasema alitumia vifaa vya baiskeli, tochi, mbao na transimita, ambayo alinunua kwa gharama shilingi 100,000.

Anasema kwa kutumia roboti huyo ambaye ameshika tochi, anaweza kuwekwa mahali ambapo kuna utulivu, iwe nyumbani au porini akiwa ni mtego wa kumsimamia mwenye nia mbaya.

“Sasa hivi roboti hatoi ‘notification’(taarifa) ya aina yeyote, ila baadae nitafunga kifaa ambacho kitakuwa ‘kina –sense’ (kinahisi) mtu ambaye anapita jirani na roboti na kama amebeba silaha au la, nikiwa ndani kwenye kompyuta nayaona yote hayo,” anasema.

Anasema hivi sasa roboti huyo anaweza kutumika kama chambo, yaani kwa kumtanguliza mbele kwenye matukio ya doria au utafutaji wa wahalifu porini, kwa kumtegesha eneo la mbali kidogo ilipo transimita ambayo inamdhibiti.

“Natumia ‘transimita’ ili aweze kugeuka kulia na kushoto kwa kipenyo cha nyuzi 45 kushoto na kulia 45, lakini baadae nataka aweze kugeuka nyuzi 360, yaani azunguke pande zote,” anasema Katabazi.

“Nilifanya utafiti kwamba matukio mengi ya ujambazi, huwa hawapendi mwanga au tochi. Ikiwa kwa mbali, wanajua ni adui yao au wameonekana na askari, hivyo wataanza kushambulia eneo lililo na mwanga, roboti huyu anaweza kutumika kama mtego wa kuwaonyesha askari waliojificha umbali kadhaa kujua sehemu fulani walipo majambazi.”

UBIA NA COSTECH

Katabazi anasema, kwamba baada ya kutengeneza roboti huyo, alishauriwa kwenda Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kwa ajili ya kupata ushauri na kuendeleza zaidi ubunifu wake.

“Nilipokwenda COSTECH walinishauri kila siku niwe naenda pale nafanya ‘project’ (mradi), lakini kwa kuwa inanipasa nitafute kipato, kushinda pale kila siku nikawaza nitakula nini nimepanga, mbali na ubunifu hii bado ninafanya shughuli ndogondogo za kujitafutia kipato,” anafafanua Katabazi.

NDEGE ISIYO NA RUBANI

Anasema awali baada ya kubuni ndege isiyokuwa na rubani, alikwenda katika Wizara ya Maliasili na Utalii, ambalo walimshauri kutekeleza mambo kadhaa.

“Nilibahatika kuonana na wakubwa kadhaa wizarani na kutoa ‘presentation’ (uwasilisho wa kitaaluma) na walinipeleka mbugani Arusha, nikaangalia ndege kama hizo zinavyoruka, changomoto ninapoambiwa niende huko kwa kutumia gharama yangu,” anasema.

Anasema ili kutimiza taratibu za masafa kwa kuwa anatumia transimita, alikwenda katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kutoa taarifa za ‘frequency’ (eneo) anayotumia katika transimita hiyo.

CHANGAMOTO NA MATARAJIO

Katabazi anasema kuwa changamoto kubwa iliyopo nchini ni uhaba wa watafiti pamoja na wabunifu, huku kukiwepo ugumu wa kuwa na mfumo wa kuendelezwa teknolojia zao.

“Tunasema tunataka Tanzania ya viwanda, lakini hatuna watafiti na wabunifu. Kukiwa na watu kama hao nchini, tutagundua mambo mengi ambayo yataendelezwa tukafungua viwanda vyetu, kiwanda kinaanza na utafiti,” anasema

Katabazi anamaliza maoni yake akisema kuwa, hivi sasa anatarajia kujiendeleza kielimu zaidi ili kufanya ubunifu mkubwa zaidi iwapo ataungwa mkono na serikali na wadau wengineo.

Kwa mujibu wa Katabazi, moja ya fani anayotamani kusoma katika shahada ya Pili ni inayohusu teknolojia ya mawasiliano ya anga.
Mpya zaidi Nzee zaidi