SERIKALI KUANZA KAMBI ZA UPASUAJI WA MABUSHA BILA MALIPO MKOANI TANGA

 


Na Rebeca Duwe Tanga


Serikali imeweka mikakati ya kudhibiti ugonjwa wa mabusha, maarufu kama ngirimaji, kwa kuandaa kambi maalumu za uchunguzi na upasuaji mdogo bila malipo katika wilaya za Handeni, Muheza na Korogwe mkoani Tanga.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda aliwataka viongozi wa serikali katika ngazi zote kuwahamasisha wananchi wenye tatizo hilo kujitokeza kwa wingi ili waweze kupata huduma hizo za matibabu bila gharama.


Alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, tangu kuanzishwa kwa kambi hizo mwaka 2009, jumla ya wagonjwa 14,454 wamepatiwa huduma nchini kote, ambapo wagonjwa 1,517 kati yao wanatoka mkoani Tanga.


Kupitia kambi hizo, wananchi watapata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa awali na wale watakaobainika kukidhi vigezo vya kitabibu watapatiwa huduma ya upasuaji mdogo.


RATIBA YA KAMBI ZA MATIBABU MKOANI TANGA


Balozi Batilda alieleza kuwa huduma hizo zitatolewa katika hospitali zifuatazo:


Hospitali ya Wilaya ya Handeni: Kambi itaanza Novemba 16 hadi 22, 2026, katika eneo la Mkata, wilayani Handeni.


Hospitali ya Wilaya ya Muheza: Huduma zitatolewa kuanzia Novemba 23 hadi 30, 2026.


Hospitali ya Wilaya ya Korogwe: Tarehe ya kuanza kwa kambi hiyo itatangazwa baadaye.


Alisisitiza kuwa wananchi wenye tatizo la mabusha au ngirimaji hawapaswi kutumia njia zisizo salama za matibabu, kujificha au kushindwa kutafuta huduma kutokana na hofu, aibu na unyanyapaa.


Aliongeza kuwa kambi hizo zitafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na wadau wengine wa sekta ya afya.


MABUSHA YANATIBIKA KWA UPASUAJI MDOGO


Kwa upande wake, Afisa Mipango wa Wizara ya Afya, Mohamed Nyati, alisema ugonjwa wa mabusha au ngirimaji unatibika kupitia upasuaji mdogo.


Alifafanua kuwa upasuaji huo ni njia ya matibabu inayotumika kudhibiti tatizo hilo, huku akiwataka wananchi kutokubali taarifa potofu na imani zisizo sahihi zinazoweza kuwajengea hofu na kuwazuia kutafuta matibabu.


Naye Mratibu wa Magonjwa ya Matende na Mabusha kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Gulinja Antony, alieleza kuwa dalili kuu ya ugonjwa huo ni kujaa kwa maji kwenye mfuko unaohifadhi korodani.


Alisema hali hiyo hujitokeza taratibu katika hatua na nyakati tofauti, na inaweza kuchukua kati ya miaka 10 hadi 15 kabla ya kubainika wazi.


Dkt. Antony alisisitiza kuwa mtu yeyote atakayebaini dalili hizo anapaswa kufika katika kituo cha kutolea huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu mapema ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.


Wito kwa wananchi: Wananchi wa Handeni, Muheza na Korogwe wenye tatizo la mabusha wanahimizwa kutumiab fursa hii kujitokeza hospitalini kwa uchunguzi na kupata huduma za matibabu bila malipo.


Afya ni mtaji. Usifiche tatizo, tafuta matibabu.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi