Kiungo wa Azam FC na Taifa Stars Himid Mao ‘Ninja’ amesema katika maisha yake hakuwahi kufikiria kama kuna siku atakuja kulipwa kutokana na kazi ya mpira licha ya kuupenda mchezo huo toka moyoni.
Himid ambae ni mtoto wa nyota wa zamani wa Pamba FC na Taifa Stars Mao Mkami amesema, hata wakati yupo shule, alikuwa anasoma lakini hakuwa akifikiria kuja kufanya kazi baadae itakayotokana na kuwa msomi.
“Tangu nikiwa mdogo nimekuwa napenda mpira na upo moyoni mwangu lakini sikufikiria mpira utakujakuwa kazi yangu, lakini mpira ni kitu ambacho nakipenda chochote nachofanya nafikiria mpira kwa hiyo sikuwahi kufikiria hata kama ningekujakufanya kazi nyingine, lakini sikuwahi kufikiria kama nitakuja kulipwa kupitia mpira.”
“Wakati nasoma shule, sikuwahi kufikiria nisome ili nijekuwa mtu fulani zaidi ya kufikiria mpira.”
Mei 1, 2017 Himid Mao alienda nchini Denmark kwa ajili ya kufanya majaribio kwenye klabu ya Randers inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo.
