Na Rebeca Duwe Tanga
Mfumo wa Maktaba Mtandao umeanza kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma za maktaba nchini, huku ukitarajiwa kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa taarifa na kurahisisha mawasiliano kati ya mifumo mbalimbali ya serikali na taasisi za elimu.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, amesema mfumo huo umejengwa kwa kuzingatia umuhimu wa mifumo ya serikali kusomana, jambo ambalo limekuwa likisisitizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Ruzegea amesema tayari Maktaba Mtandao ina uwezo wa kuhusishwa na mifumo mbalimbali ya serikali, ikiwemo mifumo ya malipo ya serikali, madeni ya serikali pamoja na mifumo inayohusiana na sekta ya elimu, ikiwemo mfumo wa takwimu unaosimamiwa chini ya Wizara ya Elimu.
Amesema kuunganishwa kwa mifumo hiyo kutasaidia kurahisisha upatikanaji na matumizi ya taarifa, huku wananchi na wadau wa huduma za maktaba wakinufaika zaidi na teknolojia katika kupata huduma.
Dkt. Ruzegea ameyasema hayo alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu kuanzishwa na kuanza kutumika kwa Maktaba Mtandao katika viwanja vya Usagara, ambako kulikuwa na Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.
Watunzi wa vitabu watakiwa kuwasilisha machapisho
Katika hatua nyingine, Dkt. Ruzegea amewataka waandishi na watunzi wa vitabu, majarida na machapisho mengine kuhakikisha wanawasilisha kazi zao katika Maktaba Kuu ya Taifa ili kupata namba ya utambulisho na kuwezesha machapisho hayo kuhifadhiwa kama sehemu ya kumbukumbu za taifa.
Kwa mujibu wa utaratibu huo, mwandishi anatakiwa kuwasilisha nakala mbili za chapisho lake. Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya teknolojia na kuongezeka kwa matumizi ya mifumo ya kidijitali, watunzi wanatakiwa pia kuwasilisha nakala ya kidijitali (soft copy) ya chapisho husika.
Dkt. Ruzegea amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha machapisho yanayotengenezwa nchini yanahifadhiwa kwa njia salama na yanaendelea kuwa sehemu ya hazina ya maarifa na kumbukumbu za Tanzania.
Kongamano la huduma za maktaba kurejea
Aidha, Dkt. Ruzegea amesema Bodi inatarajia kuandaa kongamano kubwa la huduma za maktaba, ambalo limekuwa likifanyika kila mwaka lakini lilisimama kwa kipindi cha miaka miwili.
Amesema kongamano hilo litakuwa na nafasi ya kujadili na kuendeleza huduma za maktaba nchini, huku Bodi ikitarajia kufanya urasimishaji wa Maktaba Mtandao, badala ya uzinduzi.
Amesema sababu ya kufanya urasimishaji badala ya uzinduzi ni kwamba huduma hiyo tayari imeanza kutumika na wananchi wanaendelea kunufaika nayo.
Chuo cha Ukutubi chafungua milango kwa Watanzania
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka, Bertha Mwaihojo, amewakaribisha Watanzania kujiunga na chuo hicho, akieleza kuwa ni miongoni mwa vyuo vikongwe nchini vinavyotoa mafunzo katika eneo la ukutubi na uhifadhi wa nyaraka.
Mwaihojo amesema chuo hicho kinaendeshwa na Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania na kinatoa mafunzo katika ngazi ya cheti na stashahada katika fani za ukutubi, uhifadhi wa nyaraka pamoja na utunzaji wa kumbukumbu.
Amesema katika kuendana na mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia, chuo hicho kinatarajia kuanzisha kozi mpya katika mwaka huu wa masomo, zikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Business Information Technology.
Kwa mujibu wa Mwaihojo, chuo hicho kwa sasa kina kampasi mbili nchini, ambazo ni Bagamoyo na Dar es Salaam, hatua inayowapa fursa Watanzania kupata mafunzo katika eneo la ukutubi, uhifadhi wa nyaraka na teknolojia ya taarifa.
Teknolojia kuongeza ufanisi wa huduma za maktaba
Kwa ujumla, kuanza kutumika kwa Maktaba Mtandao kunaweka msingi wa kuifanya huduma ya maktaba iendane zaidi na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
Mfumo huo unatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa taarifa, kuhifadhi machapisho kwa njia ya kidijitali na kuongeza fursa kwa wananchi kupata maarifa bila kutegemea zaidi huduma za maktaba za kawaida.
Hatua hiyo pia inaipa Tanzania nafasi ya kuendelea kujenga mfumo wa kisasa wa kuhifadhi na kusambaza maarifa, sambamba na jitihada za serikali za kuunganisha mifumo na kuongeza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

