WADAU WATAKA ELIMU ZAIDI KULINDA MIUNDOMBINU YA SERIKALI


Na Rebeca Duwe, Tanga


Serikali imetakiwa kuimarisha elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya umma, huku ikisisitizwa kuwepo kwa usimamizi madhubuti wa sheria zinazosimamia biashara ya chuma chakavu ili kuzuia mali za serikali kuibiwa na kuingia kwenye biashara hiyo.



Wito huo umetolewa na Johannes Alexander Chacha, Mkurugenzi wa Migungani Company Limited, kampuni ya jijini Tanga inayojihusisha na ukusanyaji na urejelezaji wa taka mbalimbali, ikiwemo chuma chakavu, mafuta machafu na chupa za plastiki.


Chacha amesema elimu kwa jamii ni nyenzo muhimu katika kulinda miundombinu ya taifa, hasa reli, mabomba ya maji na miundombinu ya umeme, ambayo baadhi yake imekuwa ikikabiliwa na vitendo vya uharibifu na wizi.


Amesema pamoja na wafanyabiashara halali kufuata sheria na kuwa na vibali vinavyohitajika, bado hukutana na changamoto pale wanapokutana na mali ambazo hazijulikani wazi kama ni za serikali au binafsi.


«“Naiomba serikali isimamie vema sheria zilizowekwa katika biashara hii ya taka za urejelezaji, kwani itasaidia kuwatambua wale wanaofanya biashara hii kinyume cha sheria,” alisema Chacha.»


Ulinzi wa miundombinu ni jukumu la pamoja


Kwa mujibu wa Chacha, utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu kutambua na kulinda mali za serikali unaweza kusaidia kupunguza matukio ya uharibifu wa miundombinu na pia kuwawezesha wafanyabiashara wa chuma chakavu kufanya shughuli zao bila kuingia katika migogoro isiyohitajika.


Amesema serikali inapoweka mifumo mizuri ya utambuzi na usimamizi wa mali zake, inakuwa rahisi pia kuwabaini watu wanaojihusisha na biashara haramu ya mali za umma.


Aidha, Chacha ameishukuru serikali kwa kuwapa nafasi wadau wa ndani kushiriki katika shughuli zinazohusiana na miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa mkoani Tanga, akitolea mfano mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki unaoendelea katika eneo la Chongoleani.


Amesema Migungani Company Limited imekuwa sehemu ya shughuli za kiuchumi mkoani Tanga kwa zaidi ya miaka mitano, ikichangia maendeleo kupitia ajira, ulipaji wa kodi na shughuli za urejelezaji wa taka.


Gharama za vifaa vya usalama kazini


Kwa upande wake, Afisa Rasilimali Watu wa Migungani Company Limited, Janeth Mirumbe, ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za vifaa vya kujikinga na ajali kazini, akisema bei zake ni kubwa na zinaongeza gharama za uendeshaji kwa kampuni.


Mirumbe amesema kampuni ina wajibu wa kuhakikisha wafanyakazi wake wanapatiwa vifaa stahiki vya usalama, lakini gharama kubwa za vifaa hivyo huathiri bajeti ya kampuni.


Pia amesisitiza umuhimu wa serikali kuimarisha utambuzi wa mali za umma, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza migongano inayoweza kujitokeza mara kwa mara katika biashara ya chuma chakavu.


Urejelezaji wachangia usafi wa Tanga


Mirumbe amesema pamoja na kuwa biashara ya urejelezaji ni chanzo cha kipato kwa kampuni na wananchi, pia ina mchango mkubwa katika usafi na uhifadhi wa mazingira.


«“Pamoja na kwamba kazi hii inatuingizia kipato, pia inasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza, kama si kuondoa kabisa, taka katika mazingira na kuyaacha yakiwa safi na salama. Wananchi wameichangamkia sana fursa hii,” alisema.»


Amesema kuongezeka kwa mwamko wa wananchi katika kukusanya na kuuza taka zinazoweza kurejelezwa kunasaidia kupunguza taka katika maeneo mbalimbali ya jiji na wakati huo huo kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi.


Ajira kwa vijana


Naye mfanyakazi wa Migungani Company Limited, Godlav Mollel, ameishukuru kampuni hiyo kwa kutoa ajira kwa vijana, akisema kazi hiyo imekuwa mkombozi kwake na kwa wengine wengi.


Mollel amesema kupitia ajira hiyo anapata kipato kinachomwezesha kuhudumia familia yake na kutekeleza majukumu mengine ya kijamii na kiuchumi.


Wito wa ushirikiano


Kwa ujumla, wadau hao wameeleza kuwa mafanikio katika kulinda miundombinu ya serikali yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, wananchi na wafanyabiashara wa chuma chakavu.


Wamesisitiza kuwa elimu kwa jamii, usimamizi wa sheria na utambuzi sahihi wa mali za serikali ni miongoni mwa hatua muhimu zinazoweza kusaidia kupunguza uharibifu wa miundombinu ya umma, huku biashara ya urejelezaji ikiendelea kuwa chanzo cha ajira, usafi wa mazingira na mchango katika uchumi wa taifa.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi