Ngoma aitosa Simba

Dar es Salaam. Mshambuliaji nyota wa Yanga, Donald Ngoma amesema kuwa hana mpango wa kujiunga na klabu ya Simba mara mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa mwezi ujao.

Ngoma amesema hayo kufuatia uvumi kuwa kutoonekana katika kikosi cha timu hiyo kumetokana na mkakati wake wa kujiunga na wapinzani wa jadi wa Yanga.

Ngoma ambaye ni majeruhi kwa sasa amesema kuwepo kwake nje kumetokana na kuumia na si vinginevyo na wala hana mgomo wa kuichezea timu hiyo kama inavyosambazwa na watu mbalimbali.

" Yapo mengi yamesemwa kuhusiana na mimi, mengi siyo kweli, kazi yangu ni mpira na mchezaji yoyote huwa anapenda kucheza na wala si kukaa benchi, mimi no mgonjwa na ninaangaika kujitibu,"

"Naomba nisihusishwe na Simba au timu yoyote, ni bado mchezaji halali wa Yanga na naheshimu mkataba wangu,"  alisema Ngoma.

Amefafanua kuwa uongozi wa klabu hiyo umempa ruhusa ya kupumzika na wala hajatoroka kwenda Afrika Kusini kutafuta timu zaidi ya kufuata matibabu ya kisasa.

Mchezaji huyo kutoka Zimbabwe amesema kuwa mpaka sasa hajasaini mkataba mpya na klabu hiyo pamoja na kuwa tayari kufanya hivyo endapo watakubaliana na masharti yake.

"Siwezi kusema kama nitaondoka au la, itategemea maamuzi ya wakati huo na hasa maamuzi ya uongozi, kwa sasa nimepata nafuu na nitaanza mazoezi," alisema
Mpya zaidi Nzee zaidi